Header Ads

Watu 17 wauawa shambulizi la hoteli



https://ichef.bbci.co.uk/news/660/cpsprodpb/5DB7/production/_97319932_police.jpg

OUAGADOUGOU- WATU 17 wameuawa na wengine nane wamejeruhiwa, katika shambulio la kigaidi lililotekelezwa na watu wanaodaiwa kuwa magaidi mjini hapa.
Watu walioshuhudia wamenukuliwa wakisema kwamba, watu watatu waliokuwa na bunduki waliwafyatulia risasi wateja waliokuwa nje ya hoteli moja na mgahawa.
Eneo la katikati mwa jiji limezingirwa na maofisa wa jeshi na ubalozi wa Marekani mjini hapa, umewatahadharisha raia wake wasiende eneo hilo.
Watu 30 waliuawa katika shambulio la kijihadi katika mgahawa mdogo ulio karibu na mji huu mnamo Januari mwaka jana.
Kuna wasiwasi kwamba, shambulio hilo huenda limetekelezwa na moja ya washirika wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda ambao bado wanaendesha shughuli zao katika eneo la Sahel.
Waziri wa Mawasiliano nchini, Remis Dandjinou amesema haijabainika ni washambuliaji wangapi hasa waliohusika.
“Wamejibanza katika sehemu moja ya jumba waliloshambulia. Maofisa wa usalama wanaendesha oparesheni ya kuwafurusha,” alisema kwenye televisheni.
Ufyatuaji wa risasi ulianza muda mfupi majira ya usiku wa kuamkia leo, katika barabara yenye shughuli nyingi ya Kwame Nkrumah. Maeneo mawili, Hotel Bravia na Aziz Istanbul Restaurant, yanaonekana kulengwa na washambuliaji.
“Shambulio lilisababisha vifo vya watu 17, ambao uraia wake bado haujathibitishwa, na wanane wamejeruhiwa,” taarifa ya Serikali iliyonukuliwa na shirika la habari la AFP inasema.
Hospitali moja mjini humu, ilisema mmoja wa waliouawa ni raia wa Uturuki.
Shambulio hilo linakaribiana sana na shambulio lililotekelezwa Januari 2016, ambapo watu wenye silaha walishambulia hoteli ya Splendid Hotel na mgahawa wa karibu wa Cappucino, pia katika barabara ya Kwame Nkrumah Avenue.
Watu zaidi ya 170 walishikwa mateka na 30 wakauawa. Al-Qaeda walikiri kuhusika.
Burkina Faso inapatikana katika eneo la Sahel, ambalo linajumuisha pia nchi ya Mali ambapo makundi ya Kiislamu yamekuwa yakitekeleza mashambulio tangu mwaka 2012.
BBC

No comments

Powered by Blogger.