Header Ads

Kagame aapishwa urais Rwanda



https://ichef-1.bbci.co.uk/news/660/cpsprodpb/ED47/production/_97434706_kagame.jpg

KIGALI- RAIS Paul Kagame ameapishwa rasmi kuliongoza taifa kwa muhula wa tatu wa miaka 7, baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ambayo yataruhusu muhula wa uongozi kuwa miaka saba.
Katika sherehe hizo zilizofanyika jana katika uwanja wa taifa wa Amahoro jijini hapa, marais 20 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika walifika na kushuhudia shughuli hiyo ya uapishaji.
Kuapishwa kwa Kagame, kunafuatia ushindi alioupata katika uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa Julai, ambapo alipata ushindi wa asilimia 98 ya kura zote zilizopigwa na kuwaacha mbali wapinzani wake, Philippe Mpayimana na Frank Babineza waliopata asilimia 1 ya kura zote.
Kwa upande wa viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya iliwakilishwa na Rais Uhuru Kenyatta ambaye naye alishinda uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 54 dhidi ya 44 za Raila Odinga.
Uganda iliwakilishwa na Rais Yoweri Museveni, huku taifa jipya katika jumuiya hiyo ya EAC, Sudan Kusini likiwakilishwa na Rais wake, Salva Kiir, huku Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza akishindwa kuhudhuria sherehe hizo kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.
Tanzania iliwakilishwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye alihudhuria kwa uapishaji huo kwa niaba ya Rais wa sasa, Dk John Magufuli.
Aidha, sherehe hizo zilihudhuriwa na marais wastaafu wa mataifa ya Afrika wakiongozwa na Olusegun Obasanjo kutoka Nigeria, pamoja na Festus Moghae wa Botswana.

No comments

Powered by Blogger.