Bunge la Iran lapitisha muswada kuboresha makombora

TEHRAN- Bunge
la Iran, limepitisha muswada wa kutenga zaidi ya dola za Marekani milioni 500
(sh trilioni 1.1), kwa ajili ya mradi wake wa kuboresha makombora.
Iran inajibu
vikwazo vya karibuni kabisa, vilivyowekwa na Marekani dhidi yake kutokana na
programu hiyo.
Vyombo vya
habari nchini, vinasema fedha hizo zinakusudiwa kupambana na vile vilivyoitwa
vitendo vya kigaidi vya Marekani katika Mashariki ya Kati.
Muswada huo utaweka
vikwazo dhidi ya wanajeshi pamoja na maofisa wa ujasusi wa Marekani.
Mpatanishi
mkuu wa Iran katika mazungumzo kuhusu mradi wake wa nyuklia, Abbas Araqchi,
amesema muswada huo mpya umeungwa mkono na Wizara ya Mambo ya Nje, na kwamba
hauendi kinyume na makubaliano ya mwaka 2015, yaliyozuia mradi wa nyuklia wa
Iran.
Makubaliano
kuhusu programu ya nyuklia kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani
ikiwemo China, Urusi na Uingereza, yanaonekana kwa kiwango kikubwa kama njia
mwafaka ya kuizuia Iran kuunda zana za nyuklia.
Makubaliano
hayo yalisababisha vikwazo vibaya kwa uchumi wa Iran kuondolewa, ili nchi hiyo
ipate kupunguza programu zake za nyuklia.
BBC
No comments