Header Ads

Upigaji kura ulikuwa wa kuridhisha Kenya - Mbeki



https://buzzkenya.com/wp-content/uploads/2017/08/Mbeki-speaks.jpg

NAIROBI- KIONGOZI wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika (AU), Thabo Mbeki, amesema shughuli ya upigaji kura nchini ilikuwa ya uwazi na wameridhishwa.
Licha ya upigaji kura kuwaridhisha, Mbeki alisema kulikuwa na changamoto kadhaa kama vile, kufanana kwa ukaribu zaidi kwa rangi mbili za karatasi ziliyokuwa zikitumika kupigia kura lakini tatizo hilo lilitatuliwa na maofisa wa tume kwa kuwasaidia raia kutofautisha rangi hizo..
Kiongozi huyo ambaye ni rais wa zamani wa Afrika Kusini, ameipongeza Serikali na Tume ya Uchaguzi na Mipaka Kenya (IEBC) kwa kuhakikisha wafungwa walipiga kura.
“Tunafahamu kwamba IEBC bado inahesabu na kukagua matokeo. Shughuli ya uchaguzi bado inaendelea, hivyo bado ni mapema,”
“Hata hivyo, waangalizi wa AU wanafurahi kwamba uchaguzi ulikuwa wa amani, siku ya uchaguzi watu walifika kwa wingi, na waliruhusiwa kupiga kura kwa kufuata taratibu za uchaguzi Kenya na zinazokubaliwa na AU,” alisema Mbeki.
Aidha, Mbeki aliongeza kuwa waangalizi hao wanaweza kusema kusema shughuli walizohesabu, upigaji kura na upeperushaji wa matokeo, vilitimiza viwango vya ubora vya Kenya na AU.
Alisema wamepokea malalamiko kuhusu upeperushaji wa matokeo na kutoa mwito kwa wadau kutumia mifumo wa kisheria iliyopo.
Mbeki alisema maofisa wa juu kutoka Muungano wa Upinzani nchini (NASA), walikutana na waangalizi wa AU na kuwapa ripoti kuhusu madai ya udukuzi wa mitambo ya IEBC.
Mara baada ya maofisa hao kuwasilisha madai hayo, Mbeki alieleza kuwa waliamua kuwahoji kuwa walipata vipi nyaraka hizo walizokuwa nazo za madai ya udukuzi.
“Maofisa hao wa NASA walijibu kuwa, walipewa ‘ufunguo’ fulani na IEBC wa kuweza kuingia kwenye seva. Hata hivyo, tuliwaambia kwamba, kwa kufuata fomu 34A itawezekana kwa kila mtu kubaini matokeo halisi,” alisema Mbeki.
Upinzani ulitilia shaka uhalisia wa fomu hizo na kusema katika baadhi ya vituo vya kupigia kura hawakuwa na maajenti na katika baadhi, maajenti wao walizuiwa kuingia.
Aidha, upinzani ulisema huenda fomu 34A katika baadhi ya vituo zilifanyiwa mabadiliko.
Kwa upande mwingine, Mbeki alibainisha kuwa wao kama waangalizi wa AU hawawezi kuzungumzia madai ya upinzani kwamba mitambo ya IEBC ilidukuliwa na kuongeza kuwa jukumu lao ni kuangalia shughuli ya uchaguzi inavyofanyika.
“Sisi si wachunguzi wa uchaguzi. Iwapo tungeona kitu kikifanywa vibaya, kinyume na sheria za Kenya na viwango vya AU, basi hapo tungeingilia kati,”
“Katika baadhi ya visa, NASA wamewasilisha malalamiko kwetu kuhusu uchaguzi, mfano kupatikana kwa usajili wa wapiga kura na usalama na kusafirishwa kwa maofisa takriban 40 wa polisi kwenda kwingine,”
“Tuliangazia hayo, na baadhi tukawapasha IEBC kuhusu malalamisho ya usajili na kuhusu polisi tukawasiliana na kukutana na Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang'I,” alisema Mbeki.
BBC

No comments

Powered by Blogger.