Header Ads

UN yakataa ombi la Raila kuchunguza matokeo ya uchaguzi Kenya



https://ichef.bbci.co.uk/news/660/cpsprodpb/10A0E/production/_97401186_railaz.jpg

NAIROBI- UMOJA wa Mataifa (UN), umekataa ombi la kiongozi wa upinzani nchini, Raila Odinga kukagua matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8, mwaka huu.
Msemaji wa UN, alikataa ombi hilo akisisitiza taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Gutierrez ambayo amewataka viongozi wa Kenya kusuluhisha mgogoro wowote wa uchaguzi huo katika taasisi zinazofaa Kikatiba.
UN imesema kuwa utatazama mpango mpya wa Raila, ambao anapanga kutangazwa leo.
Wiki iliyopita, kiongozi huyo wa NASA alitoa mwito kwa Umoja wa Mataifa kukagua matokeo hayo ya uchaguzi uliokamilika.
Akizungumza na gazeti la Financial Times, Raila alisema kuwa ana ushahidi wa kuthibitisha kwamba uchaguzi huo wa urais ulifanyiwa udanganyifu.
“Tutauonesha ulimwengo ule mchezo uliochezwa. Kile tunachotaka ni Umoja wa Mataifa kubuni jopo la wataalam, ambalo litatusaidia kutathmini matokeo hayo,” alisema Raila.
Kiongozi huyo wa upinzani alisema kuwa, IEBC ilikuwa chini ya shinikizo kali kutoka kwa maofisa wa Serikali inayoongozwa na Rais Kenyatta.
“Kufuatia mauaji ya mtaalam wa masuala ya kiteknolojia katika tume hiyo Chris Msando, wafanyakazi wengine waliogopa.
“Kile kilichotokea kimeshinikizwa na Serikali. Siyo kuhusu mimi na wala si kuhusu Raila Odinga kutokuwa mgombea tena. Tunataka Wakenya kujua kilichofanyika, kile ambacho dunia nzima haielewi kinafanyika.
“Hakuna haja ya watu kwenda kupanga milolongo mirefu ya kupiga kura kwa saa kadhaa, ama kufanya kampeni na huku kompyuta moja katika tume ya IEBC inatumiwa kuchakachua matokeo hayo,” alisema Raila.
BBC

No comments

Powered by Blogger.