Trump amshukuru Putin kwa kufukuza wafanyakazi wa ubalozi

WASHINGTON DC- RAIS Donald Trump amemshukuru Rais wa Urusi,
Vladimir Putin kwa kuagiza kuondoka kwa wafanyakazi 755 kutoka kwenye Ofisi za Ubalozi
wa Marekani nchini Urusi.
Akizungumza
na wanahabari mjini New Jersey, Rais Trump alisema angependa kumshukuru kiongozi
huyo wa Urusi kwa kuisaidia Marekani kuokoa fedha.
Uchunguzi
unafanyika nchini kubaini iwapo kulikuwa na ushirikiano kati ya maofisa wa
kampeni wa Trump na Urusi, inayodaiwa kuingilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2016. Trump
ameushutumu uchunguzi huo.
Mwishoni mwa
Julai mwaka huu, Rais Putin alisema wafanyakazi 755 wangelazimishwa kuondoka
kutoka ofisi za kibalozi za Marekani nchini Urusi, akilipiza kisasi hatua ya Marekani
kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.
Wengi wa
wafanyakazi hao ni waajiriwa kutoka Urusi, ikiwa na maana kwamba watu ambao
watalazimishwa kuondoka nchini humo hawafiki 755.
Alisema
watatakiwa kuondoka kufikia Septemba 1 mwaka huu, na kufanya idadi ya
wafanyakazi katika ofisi za kibalozi wa Marekani kuwa 455, sawa na wafanyakazi
wa kibalozi wa Urusi walio Washington.
Wafanyakazi
katika ubalozi wa Marekani mjini Moscow, pamoja na ofisi za kibalozi katika
miji ya Ekaterinburg, Vladivostok na St Petersburg wameathiriwa.
Wakati huo
huo, Wizara ya Mambo ya Nje nchini ilitaja hatua hiyo kuwa ya kusikitisha na
isiyofaa. Lakini Trump amemshukuru Putin kwa kupunguza wafanyakazi wanaolipwa
mishahara na Serikali ya Marekani.
“Ningependa
kumshukuru kwa sababu tunajaribu kupunguza wafanyakazi wetu, na kwangu mimi
namshukuru kwamba amewafukuza watu wengi kiasi hicho,” alisema.
Aidha, Rais
Trump alisema jana kuwa alishangazwa na uvamizi uliofanywa na maofisa wa
uchunguzi nchini katika nyumba ya mwenyekiti wa zamani wa kampeni zake, Paul
Manafort iliyopo Virginia.
Mwanasheria
maalum, Robert Mueller, anayeongoza uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba Marekani
iliingilia uchaguzi wa Urusi, aliondoka nyumbani kwa Manafort mjini Alexandria
akiwa na ‘nyaraka kadhaa’ kwa mujibu wa gazeti la Washington Post.
BBC
No comments