Trump aichimba mkwara Korea Kaskazini

WASHINGTON DC- RAIS Donald Trump ameitahadharisha Korea Kaskazini
kwamba, inafaa kuwa na ‘wasiwasi sana’ iwapo itatenda lolote kwa Marekani.
Amesema
utawala wa taifa hilo utakuwa shida kubwa ‘ambayo ni mataifa machache yaliyowahi
kukumbana nayo’ iwapo ‘hawatabadilika’.
Amesema hayo
saa chache baada ya Korea Kaskazini kutangaza kwamba, ina mpango wa kurusha
makombora manne karibu na kisiwa cha Marekani cha Guam.
Akiongea
Alhamisi Bedminster, New Jersey, Trump alidokeza kuwa huenda taarifa zake
kuhusu Korea Kaskazini hazijakuwa na ukali wa kutosha, licha ya kuionya Korea
Kaskazini wiki hii kwamba itanyeshewa na ‘moto na ghadhabu’ kutoka kwa
Marekani.
Trump
alishutumu Serikali za awali za Marekani, akisema zilionesha udhaifu kukabiliana
na Korea Kaskazini na pia akashutumu mshirika wa karibu wa Korea Kaskazini,
akisema kwamba inafaa ‘kufanya juhudi zaidi’.
Alisema: “Nawaambia,
iwapo Korea Kaskazini itafanya jambo lolote hata kwa kufikiria tu kuhusu
kumshambulia mtu tunayempenda au tunayemuwakilisha au mshirika wetu au sisi
wenyewe inaweza kuwa na wasiwasi sana, sana.”
Waziri wa Ulinzi
nchini, James Mattis ametahadharisha kwamba, mzozo wa kivita na Korea Kaskazini
utakuwa na ‘madhara makubwa’ na akadokeza kwamba juhudi za kidiplomasia kwa
sasa zinaanza kuzaa matunda.
“Juhudi za
Marekani zinaongozwa na diplomasia, zina msukumo wa kidiplomasia, na zinapata
matokeo kidiplomasia,” alisema Mattis.
Hata hivyo, Korea
Kaskazini imepuuzilia mbali vitisho vya Marekani na kuziita ni ‘upuuzi’.
BBC
No comments