Wakulima waeleza ubora wa mbegu mpya ya Pamba
Msimamizi mkuu wa Kampuni ya uchambuzi wa mbegu za pamba Quton Tanzania
Limited, Pradyumanshinh Chauhan(Kulia), akitoa maelezo kwa waandishi wa habari
waliotembelea kiwanda hicho kinachohusika na uchambuzi na usindikaji mbegu za
pamba kilichopo Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
|
Mbegu mpya aina ya UKM 08 toka kampuni ya Quton, ikiwa kwenye sahani ya
maonesho, mbegu hii tayari imefanyiwa majaribio na kuwa na sifa ya kuota bila
kubahatisha nayo imekuja sokoni sasa kwaajili ya kuiondosha ile ya zamani
iliyojulikana kama UKM 91 pamoja na ile ya manyoya.
|
Mwandishi Wetu, Mwanza
WAKULIMA wa Mkoa wa Simiyu wameielezea mbegu mpya
ya Pamba ya UKM 08 isiyo na manyoya, kuwa ni bora kutokana na kuitumia na
kuongeza uzalishaji wao hivyo kuiomba serikali kuisimamia kikamilifu
kuhakikisha inalitumia na wakulima wote.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati ya ziara na wanahabari kujionea
uzalishaji wa mbegu bora Mkoani Simiyu, baadhi ya wakulima waliopanda mbegu
hiyo katika msimu wa 2016/17 walisema mbegu hiyo ina ubora wa hali ya juu sana
ukilinganisha na mbegu ya manyoya ya UK91 ambayo imekuwa ikitumika kwa miaka
26.
Mbegu ya UK91 huzalisha wastani wa kilo 300 kwa
ekari ukilinganisha na mbegu mpya ya UKM08 iliyotolewa manyoya ambayo
inazalisha mpaka kilo 1,200 kwa ekari.
Akielezea mafanikio aliyoyapata Christopher
Nkhanda, mkulima wa Kata ya Mwabusalu Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu, alisema
mbegu ya UKM 08 ni bora na yenye mavuno mengi huku akibainisha kuwa katika
ekari 27 alizolima aliweza kupata tani 17 za pamba ambao ni wastani wa kilo 600
kwa ekari pamoja na kwamba hali ya hewa ilikuwa mbaya kutokana na ukame.
Awali mavuno yalikuwa hayazidi kilo 300 hata katika
msimu ambao hali ya hewa ni nzuri na kuna mvua ya kutosha.
“Mwanzoni niliziogopa sana mbegu hizi kutokana na
kusikia maneno ya watu kuwa hazioti, hata wakati naanza kuzilima kwa majaribio
mwaka juzi watu walinicheka lakini niliona zinamafanikio makubwa ndipo
nilipoamua kuzilima kwa wingi na kufanikiwa kupata mavuno mara mbili ya yake ya
siku zote,” alisema.
Alisema katika kutumia mbegu hizo amejifunza kuwa
kutokana na ubora wake hapaswi kupanda nyingi kama walivyokuwa wamezowea mbegu
ya zamani aina ya UK 91 ambayo kwa ekari moja walikuwa wakipanda kati ya kilo
15 mpaka 20.
Lakini sasa anapanda kilo 6 tu kwa ekari na kupata
mavuno maradufu kwani mbegu hiyo ina kiwango kikubwa cha uotaji na vilevile
inapita vizuri kwenye mashine ya kupandia jambo ambalo litasaidia katika
kuongeza tija kwani mashine inapanda kwa kuacha nafasi kama inavyoshauriwa
kwenye kanuni bora za kilimo cha pamba.
Matondo Kitinya mkulima wa Kijiji cha Ikugijo
Wilaya ya Meatu, akizungumzia mbegu hiyo mpya ya UKM 08, alisema alinunua kilo
sita kwa ajili ya ekari moja kwa Sh 15,000 na kuzipanda kwa majaribio ambapo
aliweza kuvuna kiasi cha kilo 700 na kupata kipato cha shilling 900,000
kutokana na mavuno hayo.
“Ekari moja niliyolima kwa msimu uliopita nilitumia
kiasi cha Sh 180,000 kulima, kupanda, palizi hadi kuvuna na kufanikiwa kuvuna
kiasi cha kilo 700 tofauti na kilo 200 ambazo nilikuwa nikipata awali wakati
nikitumia mbegu ya UK 91,” alieleza.
Alisema mbegu ya zamani walikuwa wakipanda kiasi
cha kilo 15 hadi 20 kwa ekari moja tofauti na hizi ambazo wanapanda kilo sita
tu lakini zikiota ndani ya siku tatu japo alisema ili upate mafanikio yake ni
lazima uzipande kwa kuzingatia vipimo na mstari kwa kuwa hazihitaji kubanana na
mche mmoja hutoa vitumba 80 au zaidi.
Kwa upande wake Minza Lukomanga wa kijiji cha
Ng’obhoko wilaya ya Meatu, alisema mbegu hizo licha ya kuwa na mavuno makubwa
lakini zimekuwa rahisi kwake kupandwa kutokana na kutumia mashine ya kupandia
hivyo kuiomba serikali kuendelea kuzalisha ikiwa ni pamoja na kuwafikishia
wakulima elimu na mbegu hii.
Akizungumzia mbegu hizo, Meneja wa Kanda wa Bodi ya
Pamba Tanzania (TCB) Jones Bwahana, alisema imekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima
walioitumia na kwamba mkakati wa bodi ni kuhakikisha mpaka kufikia 2019 mbegu
hiyo ya UKM08 inalimwa katika eneo lote la uzalishaji wa pamba hapa Tanzania.
Alisema tani zaidi ya 4,000 za mbegu ya UKM08
zilizotolewa manyoya zitasambazwa katika msimu huu wa 2017/18 ikiwa ni sehemu
ya mango wa serikali kuhakikisha wakulima wote wa paamba nchini wanatumia mbegu
bora kufikia mwaka 2019.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika tangu mwaka 2010 ilitoa jukumu la uzalishaji mbegu bora aina ya UKM
08 kwa Kampuni ya Quton (T) Ltd ambazo zimekuwa zikithibitishwa na Taasisi ya
Kupima Ubora wa Mbegu (TOSCI) kabla ya kusambazwa kwa wakulima.
Mkuu wa Kampuni ya Quton (T) Ltd, Pradyumansinh
Chauhan alisema mbegu hiyo imethibitika kuweza kuhimili magonjwa kutokana
kuandaliwa katika mfumo ambao unaua vijidudu vyote vinavyosababisha
magonjwa.
Mbegu hiyo ambayo ilipatikana kutokana na utafiti
wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Ukiriguru uondolewa manyoya kwa kutumia
tindikali na baadaye kuondoa tindikali hiyo katika mbegu kwa mfumo wa mtetemo
(gravity table) ambapo upimwa na kuthibitishwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa
Mbegu (TOSCI) kabla ya kumfikia mkulima.
Alisema kwa sasa wanazalisha tani 4,000 za mbegu
wakati uwezo wao ni tani 10,000 kwa msimu na mbegu hizo kwa sasa zimeanza
kulimwa katika maeneo ya Wilaya ya Meatu, Bariadi mkoani Simiyu, Wilaya ya
Bunda mkoa wa Mara na Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.
|
No comments