Chelsea wananichukulia kama mhalifu - Costa

SAO PAULO- MSHAMBULIAJI matata, Diego Costa amesema Chelsea
wamekuwa wakimchukulia kama ‘mhalifu’ na akathibitisha kwamba bado anataka
kurejea Atletico Madrid.
Costa (28)
aliichezea Chelsea mara ya mwisho kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Mei mwaka
huu, alitumiwa ujumbe na kocha wa timu hiyo, Antonio Conte mwezi Juni kufahamishwa
kwamba hakuwa kwenye mipango ya msimu ulioanza siku juzi.
Costa alisema
sasa klabu hiyo inamshurutisha kurejea akafanye mazoezi na wachezaji wa akiba.
“Ni kwa nini
hawataki kuniacha niondoke iwapo hawanitaki? Lazima nifanye yale inanibidi
kuyafanya. Lazima nifikirie kuhusu maslahi yangu. Nimekuwa mvulana mzuri hapa
na nilijaribu kufanya kila kitu sawa. Mapenzi yangu ni kwenda Atletico,”
alisema Costa ambaye anaamini Conte ndiye anayemchongea.
“Januari,
mambo yalifanyika kati yangu na kocha. Nilikuwa nimekaribia kutia saini mkataba
mpya, lakini akasimamisha hilo. Nashuku meneja alihusika. Aliomba hilo
lifanyike.
“Mawazo yake
ni wazi na hayabadiliki. Nimeona yeye ni mtu wa aina gani. Ana mtazamo wake na
huo hautabadilika.
“Namheshimu kama
kocha. Amefanya kazi nzuri na naona hilo, lakini kama binadamu, la. Si mkufunzi
ambaye ana uhusiano wa karibu na wachezaji. Hukaa mbali. Hana sifa za kuhusiana
vyema na wachezaji,” alisema Costa.
Juni mwaka
huu, Costa alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) na Conte kufahamishwa
hangekuwa kwenye mipango ya timu hiyo.
“Sijaufuta
ujumbe huo wa simu. Watu wakinituhumu kwamba nasema uongo, naweza kuwaonesha.
Ujumbe huo ulikuwa wazi, alisema simo kwenye mipango yake na akanitakia kila la
kheri siku zijazo. Weka kikomo hapo,” alieleza Costa.
Mshambuliaji
huyo wa Hispania alipewa muda zaidi kupumzika na Chelsea mwezi uliopita, lakini
sasa anasema anaadhibiwa kwa hilo.
Anasema
anatozwa faini kwa kutokuwa kwenye klabu muda huo, na amesema anafikiria kwenda
kortini au kujaribu kumaliza sehemu iliyosalia ya mkataba wake bila ujira nchini.
“Unajua meneja
hanitaki. Nasubiri Chelsea waniachilie huru. Sitaki kuondoka. Nilikuwa na
furaha. meneja asipokutana, ni lazima uondoke,” Costa alisema.
Costa ambaye
ni mzaliwa wa Brazil lakini huchezea timu ya taifa ya Hispania, alijiunga na
Chelsea kutoka Atletico Madrid kwa pauni milioni 32 (sh bilioni 92.8) mwaka
2014.
Alikaa
misimu minne Atletico na alikuwa amedokeza kwamba huenda akarejea katika klabu
hiyo.
BBC
No comments