Bolt: Nilikaribia kulia wakati nikiwaaga wanariadha na mashabiki

LONDON- MWANARIADHA mahiri wa Jamaica, Usain Bolt amesema hakuna
wakati mgumu aliowahi kukabiliana nao maishani mwake kama alipokuwa akiaga
mashabiki wake.
Anasema wakati
‘anasema kwaheri kwa kila kitu’ na alikaribia kumwaga chozi, baada ya kufika kikomo
cha maisha ya uanariadha katika mashindano ya ubingwa wa dunia jijini hapa.
Bolt, 30,
mshindi wa medali ya dhahabu mara nane katika Olimpiki, amestaafu rasmi riadha
baada ya kung'aa na kujizolea umaarufu mkubwa.
“Inasikitisha
kwamba inanilazimu kuondoka sasa. Nilikuwa nasema kwaheri kwa mashabiki na
kwaheri kwa mashindano niliyokuwa nashiriki pia,” alisema raia huyo wa Jamaica,
ambaye alikimbia kuzunguka uwanja kuaga jana usiku wa kufungwa kwa mashindano
hayo.
Alipoulizwa
iwapo atarejea kushindana tena, alijibu: “Nimewaona watu wengi wakistaafu na
kurudi tena, halafu hali yao inakuwa mbaya zaidi au wanajiaibisha. Sitakuwa
mmoja wa watu hao.”
Bolt
alishinda shaba mbio zake za mwisho za mita 100, kisha akaumia na kushindwa
kumaliza mbio za kupokezana vijiti za meta 4x100 Jumamosi usiku.
Hii ina
maana kwamba bingwa huyo wa dunia mara 19, ambaye Lord Coe alimfananisha na
Muhammad Ali, aliondoka kwa njia isiyo ya kawaida wakati akisaidiwa kuondoka
uwanjani na wenzake, akiwa hawezi kusimama vyema wima baada ya kuumia.
“Kwangu,
sidhani mashindano haya yatabadilisha yote niliyoyafanya. Nakumbuka baada ya
kushindwa mbio za meta 100, kuna mtu alinijia na kuniambia, 'Usain, usiwe na
wasiwasi, Muhammad Ali alishindwa pigano lake la mwisho, hivyo usisikitike sana
kuhusu hilo.
“Nimedhihirisha
ustadi wangu, mwaka baada ya mwaka. Katika kipindi changu chote nilichoshiriki
mbio hizi. Nilikuwa nasema kwaheri kwa kila kitu na nilikaribia kulia.
Nilikaribia sana, lakini machozi hayakutoka,” alisema Bolt.
BBC
No comments