Zilizotufikia muda huu; Lacazzette aonekana mazoezini Arsenal # Chelsea yamnasa Rudiger

Mshambuliaji wa Olympic Lyon na Ufaransa, Alexandre Lacazzette ameripotiwa kuonekana kwenye uwanja wa mazoezi wa Arsenal ili kukamilisha usajili.
Mwandishi wa habari wa Daily Telegraph, Jason Burt, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, Lacazzette ameonekana kwenye uwanja huo kusubiri kukamilisha usajili wake na muda wowote atatangazwa rasmi kuwa mchezaji wa Arsenal.

Gazeti la Daily Mail limeripoti kuwa, klabu ya Chelsea imeingia rasmi kwenye soko la usajili wa wachezaji baada ya kukamilisha usajili wa mlinzi wa kati kutoka Roma ya Italia, Antonio Rudiger kwa ada ya pauni milioni 36 (sh bilioni 97.2).
Mjerumani huyo mwenye miaka 24, anaelekea Stamford Bridge licha ya kuwepo kwa purukushani kutoka kwa matajiri wa Manchester, Manchester City.

Bournemouth wamefanikiwa kumsajili winga kutoka klabu ya Blackburn Rovers, Conor Mahoney kwa mkataba wa miaka minne.
Kwa muda mrefu, Mahoney amekuwa akitarajiwa kujiunga na klabu ya Nottingham Forest lakini kwa sasa atajiunga na kikosi cha vijana wa chini ya miaka 23 cha timu hiyo maarufu kama Cherries. BBC

Kwa mujibu wa wavuti ya Telesport, klabu ya Crystal Palace imeamua kuachana na windo lao Mamadou Sakho wa Liverpool, baada ya majogoo hao wa Anfield kukataa kushusha bei ya usajili.
Dau la Sakho ambalo ni pauni milioni 30 (sh bilioni 81) limedaiwa kuonekana kubwa na ndiyo chanzo cha Palace kumgeukia mlinzi wa kati wa Ajax na Colombia, Davinson Sanchez (21).
Hata hivyo, kulingana na taarifa ya Mkurugenzi wa Michezo wa Ajax, Marc Overmars, mchezaji huyo anauzwa kwa kiasi cha pauni milioni 35 (sh bilioni 94.5) na amekuwa akitakiwa na timu za Real Madrid, Barcelona na Inter Milan.
No comments