Header Ads

Wasiwasi wa abiria wairudisha ndege ya Air Asia X ilikotoka



Ndege ya AirAsia X yalazimika kurudi ilikotoka kufuatia wasiwasi wa abiria
BRISBANE- NDEGE ya kampuni ya Air Asia X iliyokuwa ikielekea Kuala Lumpur, Malaysia, ililazimika kurudi nchini baada ya ndege wawili walioingia kwenye injini kuwatia wasiwasi abiria.

Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 359, ilipata matatizo baada ya kupaa siku ya Jumatatu. Abiria waliripoti kusikia kelele kubwa na kuona miale ya moto ikitoka katika mashine ya ndege hiyo, kabla ya kutua salama mjini hapa saa moja baadaye.
Mabaki ya ndege wawili yalipatikana katika barabara ya ndege hiyo, kulingana na kampuni hiyo. Abiria mmoja, Tim Joga aliliambia jarida la asubuhi la Morning Herald kuwa, alihisi milio minne ya kelele kati ya mitano na mwanga mwingi.
Abiria mwengine, Eric Lim alisema kuwa kisa hicho kilitokea muda mfupi baada ya ndege hiyo kupaa.
“Kulikuwa na miale ya moto na sauti za boom boom boom na watu wakaanza kulia na kusema ‘Mungu wangu, Mungu wangu,” Lim aliandika katika ukurasa wake kwenye mtandao wa Facebook.
Mkurugenzi wa kampuni ya Air Asia X, Benyamin Ismail alisema kuwa rubani na wafanyakazi wa ndege walichukua hatua ya kuwahakikishia usalama abiria wakati wa kisa hicho.
“Air Asia X sasa itapanga ndege maalum ya kuwasafirisha wageni wote katika ndege D7 207 inayoelekea Kuala Kumpur haraka iwezekanavyo,” alisema Ismail katika taarifa yake.
Wiki iliopita ndege ya Air Asia X, ililazimika kurudi Perth baada ya tatizo la mashine kuifanya itetemeka ‘kama mashine ya kuosha nguo’. Mapema mwezi huu, ndege ya China Eastern Airline ilitua kwa ghafla mjini Sidney baada ya shimo kubwa kuonekana katika mashine yake.
Desemba 2014, ndege ya Air Asia ilianguka katika bahari ya Java na kuwaua abiria 162, baada ya mfumo wa rada wa ndege hiyo kutofanya kazi ilipokuwa angani.
BBC


No comments

Powered by Blogger.