Tume yapunguza mishahara ya viongozi Kenya

NAIROBI-
TUME ya Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma nchini, imetangaza
kupunguzwa kwa mishahara ya maofisa wakuu wakiwemo rais na wabunge.
Mwenyekiti
wa tume hiyo, Sarah Serem ametoa mpangilio mpya wa malipo ambao anasema utaokoa
jumla ya sh bilioni 8 (fedha za Kenya) kila mwaka na kupunguza jumla ya
mishahara inayolipwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.
Tume hiyo,
imependekeza kufutiliwa mbali kwa marupurupu ya kipimo cha usafiri wa magari
kwa magavana na wabunge na badala yake hilo litakuwa likifidiwa na mfumo mpya
wa marupurupu kwa kuzingatia kanda.
Rais sasa
atakuwa akilipwa sh milioni 1.4 kwa mwezi badala ya sh milioni 1.5, wakati
naibu wake awe akilipwa sh milioni 1.2. Mawaziri watakuwa wakilipwa sh 924,000,
Spika wa Bunge sh milioni 1.1, huku magavana wa kaunti watalipwa sh 924,000.
Mabadiliko
hayo yataanza kutekelezwa tarehe 8 Agosti, 2017. Serem amesema maofisa wa Serikali
walikuwa wakitumia vibaya mfumo wa marupurupu wa kupimiwa usafiri wa magari.
Badala yake,
maofisa sasa watakuwa wakilipwa marupurupu ya kila mwezi ya usafiri kwa
kutegemea eneo anakotoka ofisa husika. Magavana na manaibu wa magavana pia
hawatakuwa wakilipwa tena marupurupu.
Wabunge,
ambao wamekuwa wakilipwa marupurupu kwa kuhudhuria vikao vya kamati mbalimbali,
pia watakosa marupurupu hayo. Viongozi wa Serikali ya upinzani bungeni, ambao
pia walikuwa wakipokea marupurupu ya majukumu maalum pia hawatalipwa tena
marupurupu hayo.
Mishahara
hiyo mipya itaanza kutekelezwa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti. Maafisa ambao
mihula yao haitakuwa imemalizika mwaka huu wataendelea kupokea mishahara yao ya
awali.
Hata hivyo,
watakaorithi nyadhifa hiyo watalipwa kwa kufuata utaratibu mpya.
Mishahara mipya:
- Rais: Sh1.4 milioni kutoka Sh1.65 milioni
- Naibu Rais: 1.2 milioni kutoka 1. 4 milioni
- Mawaziri: Sh924,000 kutoka Sh1.056 milioni
- Makatibu wa Wizara: Sh765,000 kutoka Sh874,000
- Magavana: Sh924,000 kutoka Sh1.056 milioni
- Wabunge: Sh621,000 kutoka Sh710,000
- Maspika: Sh1.155 milioni kutoka Sh1.30 milioni
- Naibu Spika: Sh924,000 kutoka Sh1.006 milioni
- Viongozi wa Serikali na Upinzani Bungeni: Sh765,000 kutoka 1.020 milioni
- Madiwani (Wawakilishi wa Wadi): Sh144,000 kutoka Sh165,000
- Mawaziri wa Serikali za Kaunti: Sh259, 875 kutoka 350,000
No comments