Tuko tayari kudhibiti matukio ovu kabla na baada ya uchaguzi - Boinnet
NAIROBI- MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Joseph Boinnet, amebainisha
kwamba maofisa wa polisi wamepata mafunzo maalum ya kudhibiti matukio yoyote
yenye viashiria ovu kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8.
Licha ya jeshi hilo kutoa ramani ya maeneo tata zaidi ambayo vurugu
zinaweza kutokea, IGP Boinnet aliongeza kuwa polisi watahakikisha kuwa sheria
na taratibu zinaheshimika ili kuepusha kutokea kwa machafuko kama yale ya
2007-08 yaliyosababisha kuuawa kwa watu 1,000 na wengine 60,000 kukimbia makazi
yao.
“Kwenye tukio ovu la aina yoyote litakalotokea nchini, mwitikio wetu
utakuwa wa haraka na wenye kuhakikisha utii wa sheria bila shuruti unafuatwa,”
alisema Boinnet.
Mkuu huyo wa polisi, amekuwa akifanya mikutano ya mara kwa mara na maofisa
wake tangu mwezi uliopita yenye lengo la kuwapatia mbinu polisi ya namna ya
kuzuia na kukabili matukio yoyote yale.
Akizungumza kwenye kipindi cha JKL show cha Citizen TV, Boinnet aliwataka
Wakenya kutumia haki yao ya kidemokrasia kupiga kura kwa amani na kushirikiana
na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Kama zilivyo chaguzi nyinginezo, lazima kutakuwa na watu ambao
hawatafurahi wakati wengine wakifurahi. Lakini kama nilivyosema, tutakuwa
tayari kwa lolote litakalotokea, siku hiyo na baada ya siku hiyo,” alisema
Boinnet.
Capital News.
No comments