Seneta aliyemnyonyesha mtoto bungeni ajiuzulu Australia
SYDNEY- SENETA
aliyeweka historia nchini kwa kumnyonyesha mtoto bungeni, Larissa Waters
amejiuzulu baada ya kugundua kwamba ana uraia wa nchi mbili.
Waters,
kutoka chama cha Greens, alizaliwa nchini Canada. Chini ya Katiba ya Australia,
mtu haruhusiwi kuwania wadhifa wowote katika Serikali ya taifa iwapo ana uraia
wa nchi mbili na zaidi.
Ijumaa
iliyopita, seneta mwingine wa chama cha Greens, Scott Ludlam, alijiuzulu kwa sababu
kama ya Waters. Wanasiasa wote wawili walikuwa manaibu viongozi wa chama hicho.
Mei mwaka
huu, Waters alipata umaarufu kimataifa baada ya kuwa mwanasiasa wa kwanza
kumnyonyesha mtoto katika bunge la Australia.
Waters
anasema aligundua hali yake ya uraia baada ya kuibuliwa kwa kisa cha Ludlam,
ambaye aligundua kwamba naye ana uraia wa New Zealand.
Huku akijidhatiti
kuzuia machozi katika kikao cha wanahabari jana, Waters alisema lilikuwa kosa
lisilo la kukusudia.
“Nilisikitika
baada ya kugundua kwamba, kwa sababu ya sheria za miaka 70 nchini Canada,
nimekuwa na uraia wa nchi mbili tangu kuzaliwa kwangu, na kwamba sheria nchini
Canada ilibadilishwa wiki moja baada ya kuzaliwa kwangu. Sheria mpya ilinitaka
kuukana uraia wangu wa Canada,” alisema Waters.
Seneta huyo
ambaye sasa ana miaka 40, alikuwa na umri wa miezi 11 alipoondoka Canada akiwa
na wazazi wake ambao ni raia wa Australia.
“Yote haya
yalitokea kabla hata sijaweza kutamka hata neno la kwanza,” alisema. Hata hivyo,
Waters, ambaye alichaguliwa mara ya kwanza 2011, amesema anakubali lawama.
Haijabainika
iwapo yeye pamoja na Ludlam, watalipa fedha ambazo wamepokea kama mshahara na
marupurupu katika kipindi ambacho wamehudumu.
Kwa mujibu
wa Katiba ya Australia, mwanasiasa ni lazima aukane uraia wake wa taifa lingine
kabla ya kuwania wadhifa wa kisiasa.
BBC.
No comments