Mbivu mbichi za dhamana ya Lissu kujulikana kesho
KESI ya uchochezi inayomkabili Mwanasheria Mkuu wa Chadema ambaye pia ni
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu itaendelea kesho
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, huku Wakili wake Fatma Karume akiwa na
imani kuwa mteja wake atapewa dhamana.
Fatma amesema endapo Mahakama hiyo haitatoa dhamana kwa Lissu, watakata
rufaa Makahama ya Rufaa.
Lissu anayetetewa na mawakili 18, anatuhumiwa kuwa Julai 17, akiwa mtaa
wa Ufipa, Kinondoni alitoa lugha ya uchochezi hali ambayo ingesababisha chuki
kwa sababu aligusa udini, ukabila na ukanda.
Julai 24, Mbunge huyo alinyimwa dhamana na kutakiwa abaki rumande hadi kesho
ambapo Mahakama itatoa uamuzi wa dhamana, kutokana na upande wa Jamhuri kuwasilisha
pingamizi.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo, baada ya mawakili wa Lissu, Fatma na
wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi na Saimon Wankyo kujibizana kwa hoja kwa zaidi
ya saa mbili.
Baada ya majibizano hayo, Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri aliahirisha kesi
hiyo hadi kesho ili apitie hoja hizo na kuziandikia uamuzi.
No comments