Maji ya Mto Msimbazi hayafai

DAR ES SALAAM- SERIKALI imechukua sampuli ya maji ya Mto Msimbazi kwa ajili
ya kuyachunguza, ili kubaini kiwango cha sumu na ubora wa maji yake kwa matumizi
ya binadamu.
Akitoa matokeo ya awali kwa wanahabari, Meneja wa Maabara ya Mazingira wa
Ofisi ya Mkemia Mkuu, Emanuel Gwae, amesema kipimo cha maji ya Mto Msimbazi,
katika eneo la Jangwani, kinaonyesha maji hayo yana kiwango cha oksijeni cha
milimita 3.3.
Amesema kiwango hicho ni kidogo na kwamba kinachohitajika ni kuanzia milimita
sita.
“Hii inaonyesha namna ambavyo maji haya yamechafuka na viumbe hai waliomo
humu hawawezi kuishi,” amesema Gwae.
Mchakato wa upimaji wa maji hayo umefanyika leo, Jumanne, Julai 11 katika
tukio ambalo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira, Luhaga Mpina alilishuhudia.
Katika hatua nyingine, Ofisi ya Mkemia Mkuu ilichukua sampuli hiyo ya maji
ambapo Waziri Mpina alishiriki kuchota maji hayo kwa ajili ya kupimwa.
Mbali na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wadau wengine waliokuwepo ni pamoja
na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bonde la Wami-Ruvu na Baraza la Usimamizi
na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC).
Chanzo; Mwananchi
No comments