Lipumba: Maalim Seif ndiye kawaponza wabunge waliofukuzwa CUF
DAR ES SALAAM- MWENYEKITI wa (CUF) anayetambuliwa
na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema wabunge
nane wa chama hicho waliovuliwa uanachama wameponzwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad.
Profesa
Lipumba ameyasema hayo leo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na
kusema Maalim Seif na yeye ana yake ya kujibu mbele za Kamati ya Maadili na
Nidhamu ya chama hicho.
“Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na kuna
wananchama wengine wengi tu ambao pia wana makosa ya kuweza kujibu mbele ya
Kamati ya Nidhamu na Maadili. Katika watu wote hao, Katibu Mkuu yumo na yeye
ndiye amewaponza hawa wabunge nane wa Viti Maalum ambao wamevuliwa uanachama,”
“Wale wabunge wengine, wala msiwe mnasikiliza
na kufuata kila anachosema Katibu Mkuu atawaponza kama alivyowaponza wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi,” alisema Lipumba.
Kwa upande
wa Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad amesema mpaka sasa
wabunge wote nane ambao wanasemakama wamefukuzwa uanachama wameamua kufungua
kesi Mahakama Kuu kupinga maamuzi feki ambayo yamefanywa na Baraza Kuu feki.
Aidha, Maalim
Seif aliiitaka Mahakama itamke kuwa hao ni wanachama halali wa CUF na wabunge
halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Baraza Kuu
halali la CUF litakutana kwa dharura kesho Ijumaa Julai 28, ili kujadili mambo
mbalimbali ambayo yanaendelea katika chama hicho na kutangaza hatua ambazo
zitafuata,” alisema Maalim Seif.
Chanzo; EATV
No comments