Header Ads

Jaji amfutia mashtaka mtu aliyemwita mbwa wake Buhari



Muhammadu Buhari in New York Sept 2016
OGUN- JAJI wa Mahakama Kuu kanda ya Ogun, amefuta mashtaka yaliyokuwa yakimkabili mtu aliyempa mbwa wake jina la Rais Muhammadu Buhari.
Mkazi huyo wa mji huu, Joachim Iroko ambaye ni mfanyabiashara, alikutwa hana hatia baada ya waendesha mashtaka wa Serikali kushindwa kuweka wazi mashtaka hayo.
Iroko ambaye awali alikamatwa na kuachiwa, alikamatwa tena na kufunguliwa mashtaka hayo ambayo yalizua mkanganyiko na maandamano ya kupinga kuminywa kwa Katiba.
Kwa wakati huo, Msemaji wa Rais Buhari, Garba Shehu alisema Rais Buhari alistaajabishwa na hatua hiyo ya Iroko kumpa jina lake mbwa na kuongeza kuwa hatua hiyo inadhihirisha ujinga wake (Iroko).
Akizungumza mara baada ya kuondolewa mashtaka hayo, Iroko aliwashukuru wale wote waliokuwa wakimpigania hadi kufikia hatua hiyo ya kuachiliwa huru.
Ilivyokuwa
Iroko anadaiwa kutembea na mbwa wake mdogo, aliyekuwa ameandikwa jina la Buhari kwa rangi kwenye pande zote za mbavu katika eneo wanaloishi watu wengi wanaomuunga mkono Rais Buhari.
Polisi walisema walilazimika kumkamata kutokana na kuhofia usalama wake, kwani wananchi wanaweza wakamdhuru endapo akiendelea kuonekana.
Hata hivyo, Iroko amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa aliamua kumuita mbwa huyo jina hilo kwani Rais Buhari ni shujaa wake na anapambana na ubadhirifu.
“Nilimwita mbwa wangu kipenzi Buhari, kwani naye Rais Buhari ni shujaa wangu. Vitu anavyovifanya vimenivutia na vinanipa hamasa zaidi,” alisema Iroko ambaye aliviambia vyombo vya habari kuwa amepokea vitisho vya kuuliwa na watu wasiojulikana.
BBC.

No comments

Powered by Blogger.