Trump aanza kuandaa fedha za kampeni ya urais 2020
WASHINGTON DC- RAIS Donald Trump ameandaa hafla ya kuchangisha fedha
ambazo zinadaiwa kuwa zitatumika kwenye kampeni za urais za mwaka 2020 katika
hafla ambayo imeandaliwa katika hoteli moja mjini hapa.
Hata hivyo,
hafla hiyo ilitiwa doa na waandamanaji ambao walimkaripia kiongozi huyo wakisema
kwa sauti ‘Aibu!’ alipowasili kuhudhuria hafla hiyo. Kwenye hafla hiyo, kila
aliyehudhuria alikuwa analipa $35,000 (sh milioni 77).
Wengi wa
waandamanaji walikuwa hawajaridhishwa na mpango wa bima ya afya wa chama cha
Republican, na walikuwa na mabango yenye ujumbe ‘Bima ya afya, na wala si
kupunguzwa kwa kodi.’
Hoja ya kwamba
hafla hiyo ilifanyika katika hoteli ya Trump International, imeibua tena
wasiwasi kuhusu muingiliano wa maslahi kati ya majukumu ya Trump kama rais na
biashara zake.
Richard
Painter, ambaye alihudumu katika ikulu ya White House kama mwanasheria
aliyehusika na masuala ya maadili wakati wa utawala wa Rais George W Bush,
amesema haikubaliki kwa rais kuonekana akifaidika kifedha kutoka kwa hafla ya
aina hiyo.
Amesema rais
huyo angechagua hoteli nyingine na wala si moja ya hoteli zake.
Lakini,
Kathleen Clark, Profesa wa masuala ya uanasheria anayeangazia fani ya maadili
katika Chuo Kikuu cha Washington mjini St. Louis, aliambia USA Today, kwamba
Trump hakuvunja sheria zozote.
Haijabainika
bado, iwapo hoteli hiyo ililipwa kuwa mwenyeji wa hafla hiyo. Maofisa wa kamati
ya taifa ya chama cha Republican walitarajia kuchangisha takriban dola milioni 10
(sh bilioni 22), na kulikuwa na nafasi 300 zilizokuwa zinauzwa.
Hata hivyo,
fedha zote hazitatumiwa kwa kampeni ya Trump 2020 - kuna nyingine zitatumiwa na
chama cha Republican. Ni jambo lisilo la kawaida kwa rais kuanza kuchangisha fedha
za kutetea kuchaguliwa tena mapema hivyo muhula wake wa kwanza.
Trump
amehudumu kama rais kwa miezi mitano pekee.
“Bila shaka
atapigania kuchaguliwa tena,” msemaji wa White House, Sarah Huckabee Sanders
aliwaambia wanahabari jana.
No comments