Bobi Wine ashinda ubunge Uganda

KAMPALA- MWANAMUZIKI
mashuhuri wa mtindo wa Afrobeats nchini, Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu Bobi
Wine, ameshinda ubunge katika uchaguzi mdogo nchini.
Wine (pichani), ambaye
aliwania nafasi hiyo kama mgombea huru, aliwashinda wagombea wengine wanne
katika jimbo la Kyadondo Mashariki katikati mwa Uganda.
Taarifa iliyotolewa
na gazeti la Serikali la New Vision, ilieleza kuwa Wine alipata kura 25,659 kati
ya kura 33,310 zilizopigwa. Gazeti hilo lilisema baada ya kutangazwa mshindi,
aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.
“Jambo langu
la kwanza ninalotaka kulifanya, ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa
Kyadondo Mashariki. Ninataka siasa zitulete pamoja kama ambavyo muziki
ufanyavyo,” alisema Wine.
Mwanamuziki
huyo alikamatwa na polisi na kuhojiwa kwa muda, kabla ya kuachiliwa siku chache
zilizopita. Kiti hicho cha ubunge kiliachwa wazi, baada ya mahakama kuamua kuwa
uchaguzi uliofanyika mapema mwaka jana haukufuata kanuni na sheria za uchaguzi.
Kiongozi wa
chama cha upinzani cha FDC, Kizza Besigye amempongeza mwanamuziki huyo kwenye
Twitter.
Bessigye aliandika
kwamba: “Ushindi mkubwa kwa Mheshimiwa Bobi Wine. Hongera - Nguvu za Raia!!
Ndio maana watu wa Wakiso hawakuruhusiwa kupiga kura mwaka 2016.”
Wine alianza
muziki mapema miaka ya 2000. Baada ya uchaguzi mkuu wa 2016, alitoa wimbo kwa uitwao
Situka, ambao maana yake ni inuka au zinduka kwa Kiluganda.
Kwenye wimbo
huo, anatoa mwito kwa raia wa Uganda kushiriki kwenye vita dhidi ya rushwa na
ukiukaji wa haki nchini mwao.
BBC
No comments