Zitto aeleza kwa nini Tanzania ni masikini
Kwanini Tanzania ni Masikini Miaka Zaidi ya 50
Baada ya Uhuru? Tumedharau Kilimo.
[Sehemu ya 1 na ya Mwisho ya Hotuba ya ndugu Kabwe
Zuberi Ruyagwa Zitto (MB) kuhusu Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
kwa mwaka 2017/18]
Mheshimiwa Spika,
Serikali yeyote makini lazima ihangaike na masuala
yanayowahusu wananchi wake walio wengi, na hapa Tanzania watu hao (walio wengi)
ni Wakulima. Hivyo basi, kipimo kikuu cha kuondoa umasikini wa Watanzania ni
kuondoa umasikini wa wakulima.
Kilimo cha pamba
Sekta ya kilimo ndio msingi wa Uchumi wa
watanzania. Waziri wa kilimo katika hotuba yake hapa ametuambia kuwa 65.5% ya
watanzania wameajiriwa kwenye kilimo au wanategemea kilimo kwa kipato chao cha
kila siku, kwamba 100% ya chakula nchi inategemewa kutoka kwenye sekta hii.
Kilimo kinachangia 29.1% ya pato la taifa (GDP), karibia theluthi moja ya
thamani yote ya shughuli za Uchumi nchini kwetu.
Hivyo basi, unapowekeza kwenye sekta ya kilimo
unawekeza kwa theluthi mbili ya watanzania. Unapokuza kilimo unakuza uchumi wa
theluthi mbili ya watanzania, na unapoacha kilimo kishuke maana yake
umewafukarisha theluthi mbili ya Watanzania.
Kwa mujibu wa wataalamu wa Uchumi, ili kupunguza
umasikini Tanzania kwa kiwango kikubwa, sekta ya kilimo inapaswa kukua kwa
asilimia zaidi ya 8% angalau kwa miaka mitatu mfululizo, na ukuaji huo uendelee
kukua kwa wastani wa 6% kwa muda miaka kumi mfululizo.
Hali ikoje nchini? Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri
wa Kilimo, kwa miaka hii mitatu mfululizo ukuaji wa Kilimo umekuwa ukishuka
nchini (Na hivyo ukuaji zaidi wa umasikini). Mwaka 2014 sekta ya Kilimo ilikua
kwa 3.4%, Mwaka 2015 Kwa 2.3% na Mwaka 2016 Kwa 2.1%.
Taarifa ya ya robo mwaka ya Benki Kuu nchini (BOT
quarterly economic bulletin) inayoishia Disemba 2016 inaonyesha tofauti na
anachosema Waziri. Kwa mujibu wa tarifa ya BOT ni kuwa sekta ya Kilimo ilikua
kwa kasi ya 0.6% tu kutoka ukuaji wa 2.3%. 65.5% ya Watanzania wote wamejiajiri
katika sekta ya Kilimo, hivyo mdororo huu ya sekta ya Kilimo kutoka ukuaji wa
2.5% mpaka ukuaji wa 0.6% ni ishara mbaya mno kwa ustawi wa zaidi ya robo tatu
ya Watanzania.
Kwa Vijijini 78% ya Watanzania wanajihusisha na
Kilimo. Hii maana yake ni kwamba wananchi wengi vijijini hawafanyi uzalishaji,
jambo hili ni hatari sana, ni dalili kuwa ufukara wa watu wetu unazidi. Ni kwa
sababu hii, pamoja na uchumi wetu kukua kitakwimu, 7% kwa mwaka, lakini bado
wananchi wetu walio wengi wanaishi kwenye dimbwi la ufukara. Maana ukuaji huo
wa Uchumi hauhusishi kilimo, hauhusishi zaidi ya robo 3 ya Watanzania.
Tunajenga uchumi unaowaacha pembeni theluthi 2 ya
watanzania wote. Ukuaji huu mdogo wa Kilimo unapaswa kuishtua Serikali kwani ni
hatari sana, ni hatari mno. Maana unajenga uchumi unaowaacha karibu zaidi ya
robo 3 ya Watanzania kwenye ufukara huko vijijini, ni uchumi unaopanua matabaka
ya mafukara na matajiri. Ndio msingi wa umasikini wa wananchi wetu miaka 50
baada ya Uhuru.
Tatizo hasa ni nini? Kwanini ukuaji wa kilimo
unashuka na hivyo umasikini wa Watanzania kuzidi? Tatizo kubwa ni sera za
Serikali pamoja na utekelezaji wake. Serikali haiwekezi vya kutosha kwenye
kilimo, Na hata ikipanga mipango juu ya kilimo haitekelezi kabisa mipango husika.
Katika bajeti ya mwaka 2015/16, bajeti ya mbolea ya
Ruzuku katika Wizara hii ilikuwa ni shilingi bilioni 78. Bajeti ya kwanza ya
Serikali ya awamu ya tano ilishusha fedha za ruzuku ya mbolea mpaka Shilingi
bilioni 10 katika mwaka wa Fedha wa 2015/16. Hii ilikuwa ishara ya dhahiri ya
kukipuuza kilimo, kuwapuuza 65.5% ya Watanzania wote, kutokujali chanzo cha
100% ya chakula chote cha Watanzania, kupuuza sekta inayochangia theluthi moja
ya uchumi wa Taifa.
Si hivyo tu, katika bajeti ya mwaka 2016/17, Bunge
liliidhinishia Wizara hii fedha za miradi ya maendeleo katika kilimo kiasi cha
bilioni 100.53. Waziri amelieleza bunge hapa kuwa mpaka Mei 4, 2017 Wizara
imepokea shilingi bilioni 3.34, sawa 3.31% ya fedha zote za maendeleo ya
kilimo. Jambo hili linasikitisha mno, ni jambo linaonyesha kuwa hatuwajali
wanyonge wa Taifa hili.
Watanzania wanyonge walikuwa na matumaini makubwa
sana na Serikali hii, Rais Magufuli alisema yeye ni rais wa wanyonge. Wanyonge
nchi hii ni wakulima. Matendo ya Serikali anayoiongoza yanaonyesha tofauti,
Serikali haiwajali wanyonge, inapuuza uchumi wa 65.5% ya wananchi wetu. Ni
vigumu kuondoa umasikini nchini ikiwa tutaendelea kuwadharau wakulima.
Kwetu sisi ACT Wazalendo tunaofuata Ujamaa wa Kidemokrasia,
Kilimo ndio sekta ya msingi, ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, ni sekta
nyeti ambayo hatutaacha kuisemea. Hivyo pamoja na kuonyesha kasoro zote hizo za
serikali, tutatumia pia nafasi hii kutoa njia mbadala za kuondoa kasoro hizo
ili kuhakikisha uchumi wetu hauwaweki kando wananchi wetu wengi.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Bungeni Dodoma
Mei 20, 2017
No comments