Polisi yaonya wanafunzi watumiao mihadarati
Kamanda wa Polisi Dodoma (RPC), Lazaro Mambosasa
DODOMA, Tanzania
JESHI la Polisi
mkoani hapa, limewatahadharisha wanafunzi wakiwemo wa vyuo vikuu wanaofanya
biashara ya dawa za kulevya na wanaotumia dawa hizo kuwa hawatakuwa salama
kwani wamejipanga kukabiliana na biashara hiyo.
Kauli hiyo imekuja
kufuatia kukamatwa kwa mwanafunzi wa uuguzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM). Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Lazaro Mambosasa alisema jana kuwa,
jeshi hilo halitaacha kuwachukulia hatua, wote wanaojihusisha na dawa hizo.
“Tutashirikisha
vyombo vyote vya ulinzi na usalama, tutawafuatilia wanafunzi na wasambazaji,
popote walipo hawatakuwa salama,” alisema.
Aliwataka wanafunzi
kuzingatia masomo na si kujiingiza kwenye biashara na matumizi ya dawa za
kulevya. Kamanda Mambosasa aliwataka wanafunzi wenye taarifa za wanaofanya
biashara hiyo au kutumia dawa hizo kutoa taarifa ili waweze kukamatwa na
kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Mwanafunzi kaenda
shuleni kusoma lakini anauza bangi ili aharibu akili za wenzake, tunaendelea
kuwabaini wanaojihusisha na usambazaji na utumiaji dawa za kulevya,” alisema.
Alisema jeshi hilo
halitaacha kuwachukulia hatua wote wanaojihusisha na biashara hiyo. Mei 9 mwaka
huu, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa kozi ya Uuguzi katika Chuo Kikuu cha Dodoma
(UDOM), Nelson Matee (24) alikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa na misokoto 826
ya bangi yenye uzito wa kilogramu 2.8
No comments