Marekani yatoa trilioni 1.15/- kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Virginia Blaser
SERIKALI ya
Marekani kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa nchi kukabiliana na Ukimwi
(PEPFAR), imeidhinisha mpango wa kuipatia Tanzania msaada wa dola milioni 526
(sh trilioni 1.15) kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.
Kupitia
msaada huo, Tanzania itaweza kuendesha mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwa
upimaji virusi vya Ukimwi, tiba kwa waathirika, kufubaza virusi hivyo na
kuongeza idadi ya watu wanaopatiwa huduma mbalimbali za kukabiliana na Ukimwi
kufikia watu milioni 1.2.
Aidha,
msaada huo unalenga kuongeza nguvu mapambano dhidi ya Ukimwi na kufikia lengo
la kuondoa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Taarifa ya
ubalozi wa Marekani nchini imesema fedha hizo zitafadhili miradi inayotekelezwa
chini mpango wa utekelezaji wa PEPFAR utakaoanza kutekelezwa Oktoba mwaka huu
hadi Septemba 2018, kukiwa na ongezeko la asilimia 12.3 zaidi ya bajeti ya
mwaka jana.
Bajeti
hiyo iliyotengwa inajumuisha pia utoaji wa huduma na matibabu kwa watoto yatima
na wale walio katika mazingira hatarishi, pamoja na kukabiliana na ukatili wa
kijinsia. PEPFAR, pia itasaidia mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume, na
kuwafikiwa walengwa 890,000.
Mpango huu
unaendeleza ubia wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika sekta ya
afya ikiwa ni pamoja na muongo mmoja wa ushirikiano uliowezesha kudhibiti kwa
mafanikio maambukizi ya VVU.
Akizungumza
kuhusu msaada huo, Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser alisema
kwamba; “Kwa pamoja tunafanya kazi, ili hatimaye kuwa na kizazi kisicho na
Ukimwi Tanzania ambacho hakutakuwa na mtu awaye yeyote atakayeachwa nyuma.”
No comments