Header Ads

FBI wamchunguza mkwe wa Trump, Kushner



Jared Kushner na mkewe Ivanka Trump

Jared Kusner na mkewe, Ivanka Trump
WASHINGTON DC, Marekani
MKWE na Mshauri Mkuu wa Rais Donald Trump, Jared Kushner anachunguzwa na shirika la ujasusi nchini (FBI), ikiwa ni miongoni mwa uchunguzi wa Urusi.

Ripoti zinasema kuwa wachunguzi wanaamini ana habari muhimu lakini sio mshukiwa wa uhalifu. FBI linachunguza hatua ya Urusi kuingilia uchaguzi wa urais wa 2016 nchini na ushirikiano wa kundi la kampeni la Rais Trump.
Rais Trump amekana madai yoyote ya kujihusisha na Urusi wakati wa kampeni. Wakili wa Kushner amesema kuwa mteja wake atashirikiana na wachunguzi hao kuhusu uchunguzi wowote.
Rais Trump ametaja hali hiyo kuwa ‘uwindaji’ mkubwa wa kiongozi katika historia ya Marekani.
Vitengo vya ujasusi vinaamini Urusi ilijaribu kukisaidia chama cha Republican kushinda uchaguzi huo, dhidi ya mgombea wa chama cha Democrat, Hillary Clinton.
Maofisa wa Marekani ambao walikataa kutajwa, waliiambia chombo cha habari cha NBC kwamba hatua ya kumchunguza Kushner mwenye umri wa miaka 36 haimaanishi kwamba wachunguzi wanamshuku kuhusu uhalifu fulani na kwamba wanataka kumshtaki.
Kwingineko, gazeti la Washington Post limeripoti kwamba wachunguzi hao walikuwa wakiangazia mikutano aliyofanya mwaka uliopita na Balozi wa Urusi nchini, Sergei Kislyak na mfanyakazi mmoja wa benki kutoka Moscow.

No comments

Powered by Blogger.