Wazazi wataka mtoto wao aitwe Allah
GEORGIA,
Marekani
WANANDOA
wawili jimboni hapa, wamewasilisha kesi mahakamani baada yao kuzuiwa kumpa
mtoto wao jina Allah.
Wizara ya Afya
ya Umma ya jimbo ilikataa kumpa msichana huyo wa umri wa miezi 22 cheti cha
kuzaliwa kwa sababu ya jina lake. Elizabeth Handy na Bilal Walk wanasema
haikubaliki kwamba sasa mtoto wao ameachwa kirasmi akiwa hana jina.
Lakini maofisa
wa Serikali wanasema jina la ukoo la mtoto huyo ZalyKha Graceful Lorraina Allah
linafaa kuwa Handy, Walk au majina yote mawili.
Allah ni
jina la Mungu kwa Kiarabu.
Shirika la
Haki za Raia Marekani (ACLU) tawi la Georgia limewasilisha kesi kwa niaba ya
familia hiyo katika Mahakama Kuu ya wilaya ya Fulton. Baba yake msichana huyo,
aliambia gazeti la Atlanta Journal-Constitution kwamba aliamua kumpa jina Allah
kwa sababu ni jina ‘adilifu’.
"Huu ni
ukiukaji wazi wa haki zetu," Walk alisema kuhusu hatua ya jimbo kukataa
kutambua jina hilo.
Hata hivyo,
mawakili wa Wizara ya Afya ya Umma ya jimbo wanasema sheria za Georgia ‘hutaka
jina la ukoo la mtoto liwe la baba au mama yake mtoto kwa ajili ya hati ya
kwanza rasmi ya kuzaliwa (kwa mtoto).’
Kwenye barua
kwa familia hiyo, maofisa wa Serikali walisema jina la ukoo la ZalyKha linaweza
kubadilishwa baadaye kupitia ombi kwa Mahakama Kuu ya jimbo.
Hata hivyo,
hilo linaweza kufanyika tu baada ya cheti cha kwanza cha kuzaliwa kwa mtoto
huyo kutolewa.
Kwa mujibu
wa kesi iliyowasilishwa kwa niaba ya familia hiyo, wanandoa hao ambao
hawajafunga ndoa rasmi wana mtoto wa kiume aliyepewa jina Masterful Mosirah Aly
Allah.
ACLU
wanasema bila kupata cheti cha kuzaliwa, itakuwa vigumu kwa wazazi hao kupata
nambari rasmi ya utambulisho kwa ajili ya kupokea huduma kutoka kwa Serikali. Wanahofia
kwamba huenda utambulisho wa msichana huyo, pamoja na haki zake kama raia wa
Marekani zikatiliwa shaka.
ACLU
wamesema hatua ya jimbo hilo kukataa kutimiza maombi ya familia hiyo ni mfano
wa serikali kuvuka mipaka na kutofuata katiba.
“Wazazi ndio
huamua jina la mtoto wala siyo jimbo. Ni jambo rahisi sana” alisema wakili wa
familia hiyo, Michael Baumrind.
No comments