Waziri Mkuu apokea taarifa ya uchunguzi kuhusu kifo cha Faru John
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea ripoti kutoka kwa Mkemia Mkuu
wa Serikali, Profesa Samwel Manyele taarifa ya Tume aliyoiunda ya kuchunguza
suala la Faru John, ofisini kwake jijjini Dar es salaam Machi 27, 2017. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU
APOKEA TAARIFA YA KIFO CHA FARU JOHN
*Ni ya
uchunguzi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa rasmi
ya uchunguzi wa kifo cha Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof.
Samwel Manyele ambaye alikuwa akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amepokea taarifa hiyo, leo (Jumatatu,
Machi 27, 2017) kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni
jijini Dar es Salaam.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri
Mkuu, Prof. Manyele amesema tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John
kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe,
damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya
mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni dume.
Prof. Manyele amesema matokeo hayo
yamethibitisha kuwa faru John alikufa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa
kukosa matunzo na uangalizi wa karibu.
“Maabara iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria,
Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania,
wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Sababu za
kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa
matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa
kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake,”
amesema.
Prof. Manyele amesema mapungufu waliyoyabaini
kutokana na uchunguzi huo ni kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru
John; kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa
Grumeti na kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya
kuhamishwa.
Mengine ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama
pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi
kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi
binafsi na uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya
uhifadhi wa wanyamapori.
“Pamoja na
kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara, hapakuwepo na
kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru
John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema Prof. Manyele katika ripoti yake.
Akizungumzia kuhusu uchukuaji holela wa sampuli za
wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi, Prof. Manyele
amesema kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli wanazochukua haziwekwi vizuri
na kwamba tume inashauri TAWIRI na TANAPA wapewe msisitizo juu ya umuhimu
wa kuzingatia majukumu yao.
Amesema kuna umuhimu wa kudhibiti watafiti na
tafiti ili kulinda taarifa muhimu za vinasaba vya wanyamapori (Genetic
information) dhidi ya mataifa mengine. “TUME inashauri maabara ya Mkemia Mkuu
wa Serikali ianzishe kitengo cha Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya
Wanyamapori (DNA Forensic Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake
iweze kufanya maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa
kimahakama katika kesi za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).
Akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu aliishukuru timu ya uchunguzi
iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi iliyoifanya ikiwemo
kuainisha udhaifu uliokuwemo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi
zake.
“Ofisi yangu itaipitia taarifa hii
ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi. Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi
karibuni ili kuonyesha Serikali imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo
yaliyotolewa.”
Alimtaka Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo
cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande, afuatilie
mapendekezo yaliyoainishwa na tume hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo.
Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba
10, mwaka jana baada ya kupokea pembe mbili za faru John na taarifa yenye
nyaraka zilizotumika kumhamisha faru huyo. Hatua hiyo
ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa ziarani mkoani Arusha, ambapo
alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru John kutoka kwenye
hifadhi hiyo.
Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao
makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na
watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni
sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, MACHI 27, 2017.
No comments