Watu 600 hawajulikani walipo Sierra Leone

FREETOWN- TAKRIBAN watu 600 wametoweka mjini hapa, kufuatia
maporomoko ya matope na mafuriko yaliyotokea katika maeneo kadhaa mjini hapa.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Rais Ernest Bai Koroma, Abdulai Baraytay,
ilieleza maporomoko hayo yaliyotokea katika baadhi ya sehemu mjini hapa
yamesababisha kutoweka kwa watu hao ambapo jana ilipatikana miili 270.
Awali, Rais
Koroma aliomba usaidizi wa dharura akisema jamii nzima ilikuwa imeangamia.
Takriban
watu 400 wamethibitishwa kufariki dunia, kutokana na maporomoko hayo ya eneo la
Regent na mafuriko yaliyotokea katika maeneo mengine mjini hapa.
Shjrika la Msalaba
Mwekundu limeonya kuwa, hakuna muda wa kutosha kuweza kuwaokoa manusura. Maziko
ya pamoja ya waathiriwa yanatarajiwa kufanyika leo ili kupunguza idadi ya miili
katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Baraytay aliiambia
BBC kwamba, miili ilikuwa ikitolewa katika matope hayo na vifusi na kuongeza
kuwa jamii nzima inaomboleza.
“Wapendwa
wengine wametoweka, takriban zaidi ya watu 600,” alisema Baraytay.
Umoja wa Mataifa
(UN) umesema kwamba, wafanyakazi wake nchini wamekuwa wakisaidia katika juhudi
za kuwaokoa manusura.
“Mikakati
inawekwa kuzuia mlipuko wowote wa magonjwa yanayosababishwa na maji kama vile
kipindupindu, homa ya manjano na kuharisha,” alisema Msemaji wa UN, Stephane
Dujarric.
Nyumba za
jamii zilizokuwa zikiishi juu ya mlima ziliangamia, baada ya upande mmoja wa
mlima wa Sugar Loaf kuporomoka kufuatia mvua kubwa mapema siku ya Jumatatu.
Waathiriwa
wengi walikuwa wakilala wakati wa mkasa huo.
Rais Koroma
alizuia machozi alipotembelea eneo la Regent siku ya Jumatatu na kusema kuwa
uharibifu huo umepita kiasi.
''Jamii
nzima imeangamia tunahitaji msaada wa dharura'', alisema.
BBC
No comments