Waandamana kushinikiza uchunguzi kifo cha ofisa IEBC

NAIROBI- WATETEZI
wa haki za kibinadamu wameandamana katika uwanja wa Uhuru Park, kushutumu
kuuawa kwa ofisa wa ngazi za juu wa Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC), Christopher
Msando.
Msando
alitoweka Ijumaa na mwili wake ukapatikana ukiwa umetupwa viungani mwa jiji hili
Jumamosi asubuhi. Mwili wake ulitambuliwa jana katika chumba cha kuhifadhia
maiti cha City.
George
Kegoro kutoka shirika lisilo la kiserikali la Tume ya Haki za Kibinadamu Kenya
(KHRC), amesema wana wasiwasi kwamba mauaji ya Msando yatazua mtafaruku
uchaguzi mkuu unapokaribia.
Waandamanaji
walibeba mabango wakihimiza umuhimu wa tume ya uchaguzi IEBC, kutoingiliwa.
Wamesema sababu
pekee ya kumuua ofisa huyo aliyekuwa akisimamia mfumo wa teknolojia wa uchaguzi
katika tume hiyo, ni kuingilia uchaguzi wenyewe na kwamba hilo huenda
likachochea ghasia.
Waandamanaji
hao walipanga kuandamana hadi ofisi za Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet na makao
makuu ya IEBC.
Mwenyekiti
wa IEBC, Wafula Chebukati, kupitia taarifa baada ya kutambuliwa kwa mwili wa Msando,
alitoa mwito kwa polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha kifo
chake.
“Tume
itamteua wakili huru wa kushirikiana na Mkuu wa Polisi katika uchunguzi.
Tunataka haki kwa Chris, Haki kwa IEBC na Haki kwa Taifa,” alisema Chebukati.
Chebukati
alimuomba mkuu wa polisi kuimarisha ulinzi kwa makamishna na maofisa wakuu wa
tume hiyo.
BBC.
No comments