Upinzani wakataa matokeo, waitaka IEBC imtangaze Raila mshindi

NAIROBI- MUUNGANO wa upinzani nchini (NASA), umeendelea
kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yanayotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na
Mipaka (IEBC) kwenye mtandao wake.
Viongozi wa
muungano wa NASA, wamesema walikutana na wakuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya na
kuwasilisha rasmi malalamiko yao kupitia barua.
Ajenti Mkuu
wa upinzani, Musalia Mudavadi, ambaye ni Naibu Waziri Mkuu wa zamani, amesema
upinzani umepata maelezo zaidi kwamba matokeo ya uchaguzi yalivurugwa baada ya
kudukuliwa kwa mitambo ya IEBC.
Wakuu wa
IEBC wamekanusha kwamba mitambo ilidukuliwa. Mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula
Chebukati amesema kulikuwa na jaribio la kudukua mitambo hiyo, lakini
halikufanikiwa.
Mudavadi
amedai mgombea wao Raila Odinga ndiye aliyeshinda uchaguzi huo.
“Tunamtaka Mwenyekiti
wa IEBC atangaze matokeo na kumtangaza Odinga na Kalonzo kama rais mteule na
naibu rais mteule wa Kenya mara moja,” alisema Mudavadi huku akiwasisitiza
Wakenya waendelee kuwa watulivu.
Kwa mujibu
wa sheria nchini, ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kutangaza matokeo au
kusambaza matokeo ambayo hayajatoka kwa tume ya taifa ya uchaguzi.
Ni tume hiyo
ya uchaguzi pekee ndiyo inayoruhusiwa kutangaza matokeo.
BBC
No comments