Header Ads

Kim Jong-un akabidhiwa mpango wa kukishambulia kisiwa cha Marekani



https://ichef.bbci.co.uk/news/624/cpsprodpb/71CD/production/_97333192_guam_map624.png

PYONGYANG- VYOMBO vya habari nchini, vimeripoti kuwa Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un amekabidhiwa rasmi ripoti ya taifa yenye mpango wa kutaka kurusha kombora hadi katika kisiwa cha Guam kilichopo eneo la pacific na kinachomilikiwa na Marekani.
Hata hivyo, ripoti hiyo imesema kuwa itachunguza vitendo vya Marekani kabla ya kuchukua hatua ya kurusha kombora hilo katika kisiwa hicho.
Wiki iliyopita, Korea Kaskazini ilionya kwamba mikakati inawekwa kushambulia eneo hilo ambalo ndegevita za Marekani zimeweka kambi na kuongeza urushianaji maneno baina ya mataifa hayo mawili hasimu.
Ripoti hiyo ya kitengo cha habari cha KCNA, ilisema Kim aliutazama mpango huo kwa muda mrefu na kuujadili na maofisa wakuu wa jeshi. Kamanda wa jeshi la kimkakati la Korea Kaskazini, sasa anasubiri agizo baada ya kuandaa shambulio hilo la Guam.
Ripoti hiyo imeongezea kwamba, Kim atachunguza mienendo ya Marekani kabla ya kutoa uamuzi wowote, hatua inayoonekana kupunguza kasi ya cheche za maeneo kati ya mataifa hayo mawili.
Mwandishi wa BBC, Yogita Limaye aliyepo mjini Seoul, anasema hatua hiyo itapunguza wasiwasi na kuzuia mgogoro wa kijeshi katika eneo la Korea.
Mwandishi mwingine ameongeza kuwa, baada ya siku kadhaa za vitisho kutoka Pyongyang, inaonekana kwamba Rais Kim sasa anataka kunyamaza na kutazama hali, lakini katika taifa lenye siri kubwa kama Korea Kaskazini huwezi kuwa na hakika.
Wachanganuzi wanasema, hali hiyo inamaanisha kwamba Pyongyang haiko tayari kutekeleza shambulio katika kisiwa cha Guam, hivyo huenda inachukua muda.
Hatua hiyo inajiri baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis kuonya kwamba shambulio lolote linaweza kusababisha vita vikali, na iwapo Pyongyang itarusha kombora kuelekea Guam basi ‘itakuwa vita’.
Amewaambia waandishi wa habari kwamba, Jeshi la Marekani litatetea taifa hilo iwapo kutakuwa na shambulio lolote wakati wowote na kutoka kwa taifa lolote.
Pia, aliwahakikisha raia wa Guam, ambapo kuna kambi za kijeshi za Marekani kwamba, takriban watu 160,000 wanalindwa na akasema iwapo kombora litarushwa ‘tutalitibua’.
BBC

No comments

Powered by Blogger.