Mugabe auza ng’ombe 600 kuisaidia AU

ADDIS ABABA-
RAIS Robert Mugabe amebainisha kwamba, Zimbabwe imeuza ng'ombe 600 na kupata dola
za Marekani milioni 1 (sh bilioni 2.2) kwenye mnada na kukabidhi fedha hizo kwa
Wakfu wa Muungano wa Afrika kusaidia kumaliza utamaduni wa kutegemea fedha
kutoka kwa wafadhili.
Rais Mugabe
alisema kuwa, yeye binafsi alitoa ng'ombe 300 kutoka kwenye zizi lake, na raia
wengine wa Zimbabwe wakaongeza ng'ombe wengine 300.
Akizungumza katika
mkutano huo, Mugabe alisema mchango huo ni mdogo tu lakini ni ishara muhimu
katika kujaribu kukomesha utegemezi wa Afrika kwa fedha za wafadhili.
“Kama
Mwafrika na mkulima, kutoa ng'ombe ni jambo la kawaida kwangu, ikizingatiwa
kwamba bara letu limebarikiwa na ng'ombe wengi na ng'ombe hutazamwa kama hazina
ya utajiri,” alisema Mugabe.
Mugabe
alikabidhi hundi hiyo ya dola milioni 1 kwa AU, wakati wa mkutano mkuu wa
viongozi wa mataifa wanachama nchini Ethiopia. Mchango huo wa Zimbabwe, unakuja
katika kipindi ambacho taifa hilo linakabiliwa na uhaba wa fedha na chakula.
Mwaka jana,
watu zaidi ya milioni 4 nchini humo walihitaji chakula cha msaada baada ya mvua
kutonyesha kwa kiwango stahiki. Hata hivyo, mwaka huu mavuno yamekuwa mengi na
taifa hilo linatarajiwa kujitosheleza kwa chakula kwa mara ya kwanza katika
miaka mingi.
Upinzani
umelaumu Serikali kwa uhaba huo wa chakula, na kusema kwamba sera yake yenye
utata ya kupokonya wazungu mashamba ilichangia kusambaratisha sekta ya kilimo.
Zimbabwe
imelazimika pia kuanza kutumia hati za dhamana baada ya kuishiwa na dola za
Marekani, fedha ambazo hutumiwa kwa biashara nchini humo. Kiwango cha juu cha
mfumko wa bei kiliilazimu Zimbabwe kuacha kutumia dola yake mwaka 2009.
Waziri wa Mambo
ya Nje wa Zimbabwe, Simbarashe Mumbengegwi alisema ng'ombe hao walitolewa na
watu waliofaidika kutokana na mageuzi katika sera ya mashamba nchini humo, kwa
mujibu wa gazeti la Serikali la Herald.
Msaada huo
ulikuwa ni ‘kuimarishwa’ kwa ahadi ya Mugabe ya mwaka 2015, kwamba angetoa
ng'ombe 300.
Kwenye
tovuti yake, Wakfu wa AU unasema huwa unaangazia mipango ya vijana na wanawake,
na kuendeleza usawa wa jinsia.
Wakati wa
kipindi chake kama mwenyekiti wa AU kati ya 2015 na 2016, Mugabe alitetea AU
iwe ikifadhiliwa na Waafrika. Kwa sasa asilimia 60% ya bajeti ya umoja huo
hutoka kwa wafadhili kutoka nje.
No comments