Hakimu ajitoa kusikiliza kesi ya Lema
ARUSHA- HAKIMU wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha,
Patricia Kisinda aliyekuwa anasikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa
Jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema dhidi ya Rais John Magufuli amejitoa baada
ya kuwekewa pingamizi kuwa ana urafiki na mke wa Lema (Neema Lema).
Hakimu huyo
ni wa pili kujitoa katika kesi hiyo, kwani Mei 29, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa
Arusha, Desderi Kamugisha pia alijitoa kwa maelezo kuwa hawezi kusikiliza kesi
zote nne zinazomkabili Lema hivyo kuwaeleza mahakimu wengine watapangiwa kesi
hiyo.
Alhamisi hii
wakati kesi ikipangwa kusomewa maelezo ya awali, Wakili wa Jamhuri katika kesi
namba 441, Sabina Silayo aliwasilisha hoja katika mahakama hiyo kuwa Hakimu
Kisinda ana urafiki na Neema.
Sabina
alieleza mahakama kuwa ana ushahidi kuwa hakimu Kisinda ana urafiki wa karibu
na mke wa Lema.
“Ombi la
Jamhuri ni kuwa hatuna imani na wewe kuendelea na shauri hili na tunaomba
ujiondoe kwa vile mke wa mshtakiwa ni rafiki wako wa karibu sana na ushahidi
huo tunao na haina pingamizi,” amesema Sabina.
Amesema
Hakimu huyo kuendelea kusikiliza kesi hiyo kutaondoa imani kwa upande wa
Jamhuri kwani huenda haki isitendeke na hivyo aliiomba mahakama ipange kesi
hiyo kwa hakimu mwingine.
Baada ya
hoja hiyo kuwasilishwa mbele ya wakili wa utetezi wa Lema, Sheck Mfinanga
aliomba mahakama kutupa hoja hiyo kwani haina uzito kwa kuwa Watanzania wote ni
ndugu na ni marafiki.
Wakili
Mfinanga amesema kesi hiyo haina urafiki hivyo kama mahakama iko kwa ajili ya
kusimamaia sheria na haki iache hakimu huyo aendelee na kesi hiyo.
Hata hivyo,
Wakili wa Serikali Sabina alijibu hoja hiyo kwa kuonyesha mashauri mbalimbali
ambayo yalionyesha kuwa kuna kanuni na sheria za mahakama kuwa endapo
itabainika kuwa Jaji au Hakimu ana uhusiano wowote na mshtakiwa au mshtaka
atatakiwa ajiondoe kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo,
kutokana na hoja hizo za pande mbili, Hakimu Patricia ametumia dakika 20
kufanya uamuzi mdogo juu ya hoja ya upande wa Jamhuri na amekubaliana ana hoja
hiyo ya kujiondoa.
Hakimu
Patricia amesema ameamua kujitoa ili kupisha haki itendeke lakini yeye si
rafiki na mke wa Mbunge bali anamfahamu tu.
Hata hivyo,
amesema rufaa juu ya uamuzi huo iko wazi na kwamba Agosti 2 mwaka huu kesi hiyo
itafikishwa mahakamani tena kwa ajili ya kupangiwa hakimu mwingine kwa ajili ya
kusomewa maelezo ya awali.
Chanzo:
Mwananchi
No comments