Header Ads

Trump alaumiwa kwa uamuzi wake



Bwana John Mahama
PARIS, Ufaransa
RAIS wa zamani wa Ghana, John Mahama amelaani uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kwa kuiondoa Marekani kwenye makataba wa Paris wa 2015 kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Mahama (pichani) alituma ujumbe wake kwa njia ya Twitter, akiutaja uamuzi wa Trump wa kujiondoa kwenye makataba huo wa mazingira kama “Jambo ambalo ni vigumu kuliamini. Ni siku ya huzuni sana katika ushirikiano wa kimataifa.”
Rais huyo wa zamani alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa dunia waliounga mkono makubaliano hayo ya kihistoria juu ya mazingira mjini Paris, akiahidi kutekeleza hatua za kupunguza hewa ya makaa duniani.
Alitwitt kwamba Marekani imejiondoa katika uongozi wake wa dunia. Trump alisema kuwa mkataba huo ‘uliiadhibu’ Marekani na utasababisha kupotea kwa mamilioni ya ajira nchini humo.
Wakati huo huo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Afrika alisema: “Mabadiliko ya hali ya hewa ni tisho kubwa la enzi yetu, Makubaliano ya Paris ni matokeo ya makubaliano mengi ya ushirikiano na utashi wa kutafuta suluhu ya pamoja ya tatizo la dunia.
Hakuna nchi moja inayoweza kuvuruga makubaliano. Wakati Marekani inajiondoa inadhoofisha mkataba huo wa kimataifa, haitauvunja,” alisema Annan.
“Kilichosalia kwa mkataba wa Paris ni kwa pande zilizosalia kuendelea kujitolea kuongeza juhudi za kutatua matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi,” Annan aliandika kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Wazee wa Afrika.
Ndani ya Marekani kwenyewe, biashara na mamlaka za majimbo zinaweza na lazima zikchukue hatua pale serikali ya shirikisho itakaojiondoa, waliongeza.


No comments

Powered by Blogger.