Ilani za uchaguzi zazua maneno Kenya

NAIROBI- MIJADALA mikali imezidi kupamba moto
kwenye ulingo wa kisiasa nchini, baada ya Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA)
pamoja na chama tawala, Jubilee, kushutumiana vikali kuhusiana na ilani.
NASA inayoongozwa na Raila Odinga, ndiyo ambao walioanzisha
mashambulizi kwa Jubilee, baada ya kudai kuwa ilani ya Jubilee ina mapungufu
mengi na isiyokuwa na maana yoyote kwa Wakenya.
Mara baada ya mashambulizi hayo, Jubilee wanaoongozwa
na Rais Uhuru Kenyatta nao walijibu shutuma za wapinzani kwa kudai kwamba
wamekuwa wakinadi malengo ambayo si ya kweli.
Awali, NASA walitoa taarifa iliyodai kwamba Jubilee
wameshindwa kuwaeleza Wakenya kuhusu wao kushindw akutekeleza ahadi zao walizotoa
kwenye ilani yao ya uchaguzi wa mwaka 2013, na kisha kudai kuwa ilani yao
(Jubilee) iliyozinduliwa Jumatatu wiki hii inaakisi ahadi nyingi zilizofeli.
Seneta wa Kisumu, Anyang’ Nyong’o ambaye
anaiwakilisha NASA, alisema kuwa Jubilee haipaswi kuaminika kuwa itaboresha
uchumi wakati utawala wao ulishindwa kusimamia uchumi huo kwa miaka yote
waliyokuwa madarakani.
“Kila sekta inapunguza wafanyakazi kuanzia kampuni
za simu, benki hadi bima. Tazama bei ya unga, mfumuko wa uchumi ambao
umesababisha mamilioni ya Wakenya kutomudu gharama za maisha,” alidai Nyong’o.
Lakini Jubilee kupitia kwa Katibu Mkuu wao, Raphael
Tuju na Naibu Katibu Mkuu, David Murathe, walipuuza shutuma za NASA na badala
yake waliwashutumu kwa kutoa ahadi zisizo za kweli kwa Wakenya kupitia ilani
yao.
“Hivi ni kweli kwamba hatuna kitu tulichokifanya? Tumefanikiwa
kutengeneza mradi mkubwa wa Standard Gauge ambao ni mkubwa kwa Afrika Mashariki
na Kati katika kipindi cha miaka mitatu tu. Wao wamechagua kutoona hata yale ya
kawaida,” alisema Tuju.
No comments