Trump kuzuru Israel chini ya ulinzi mkali
WASHINGTON
DC, Marekani
RAIS Donald
Trump anazuru Israel na maeneo ya Wapalestina leo, akiendelea na ziara yake ya
kikazi katika maeneo ya Mashariki ya Kati.
Atafika
maeneo hayo akitokea Saudi Arabia, mshirika muhimu wa Marekani, ambako alitoa
hotuba katika mkutano mkuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Trump (pichani)
anatarajiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel na Palestina katika
kipindi cha siku mbili atakazokuwa eneo hilo.
Rais huyo alisema
kupatikana kwa mkataba wa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina, yatakuwa
mafanikio makubwa, lakini hakusema mkataba kama huo unafaa kuchukua mwelekeo
gani.
Alisema
angependa pande zote mbili ziamue kuhusu mkataba huo wa amani kwa mashauriano
ya moja kwa moja.
Katika
mkutano mkuu wa viongozi wa Kiislamu na Kiarabu mjini Riyadh jana, Trump
aliwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na wanamgambo wa
Kiislamu na wapiganaji wenye itikadi kali na ‘kuwafurusha kutoka kwenye dunia
hii.’
Aliitaja
moja kwa moja Iran na kusema kwamba imekuwa ‘ikichochea mizozo ya kidini na
ugaidi’ katika kanda hiyo kwa miongo mingi.
Trump pia
alikaririwa tena akisema kwamba, anaamini amani kati ya Waisraeli na
Wapalestina inaweza kupatikana. Rais huyo amekuwa akichukuliwa kuwa muungaji
mkono mkubwa wa Israel kuliko mtangulizi wake, Barack Obama.
Amechukua
msimamo usio mkali, kuhusu suala tata la Israel kujenga makazi ya walowezi
maeneo ya Wapalestina na kudokeza kwamba upanuzi wa makao hayo na si kuwepo kwa
makao yenyewe, unaweza kuwa ndio kikwazo katika kutafuta amani.
Zaidi ya
Wayahudi 600,000 huishi katika makao makazi 140 ya walowezi ambayo yamejengwa
tangu Israel ilipotwaa maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem
mwaka 1967, maeneo ambayo Wapalestina huyachukuliwa kuwa sehemu ya ‘taifa
litakaloundwa’ la Wapalestina.
Makazi hayo
ni haramu chini ya sheria za kimataifa, lakini Israel hupinga hilo.
Rais huyo
pia ametoa ishara za kukanganya kuhusu mji wa Jerusalem, na kuahidi kuhamishia
ubalozi wa Israel mjini humo kutoka Tel Aviv, hatua iliyowakera Wapalestina
lakini ikawafurahisha zaidi Waisraeli.
Hata hivyo,
baadaye alionekana kulegeza msimamo huo, na Waziri wa Mambo ya Nje, Rex
Tillerson juzi aliambia NBC News kwamba Trump bado analitafakari jambo hilo.
Mzozo kuhusu Jerusalem
Israel
huuchukulia mji wote wa Jerusalem kuwa mji wake mkuu, huku Palestina ikichukulia
maeneo ya Mashariki ya mji huo kuwa makao makuu yake.
Jamii ya
kimataifa haijatambua umiliki wa Israel kwa mji wa Jerusalem na mataifa mengi
yana ofisi za kibalozi mjini Tel Aviv. Kumekuwa na wasiwasi kidogo Israel kabla
ya ziara ya Trump kutokana na baadhi ya matamshi ya maofisa wake.
Waziri Mkuu
wa Israel, Benjamin Netanyahu amepuuza maneno ya Tillerson kwamba kuhamishwa
kwa Ubalozi wa Marekani kunaweza kuathiri shughuli ya kutafuta amani eneo hilo.
Ofisa wa Kibalozi
wa Marekani, naye aliwakera Waisraeli aliposema kuwa Ukuta wa Magharibi, moja
ya maeneo matakatifu zaidi katika dini ya Kiyahudi haumo “katika maeneo yenu
(Waisraeli) bali ni sehemu ya Ukingo wa Magharibi.”
White House
baadaye ilisema tamko la ofisa huyo wa kibalozi ‘hayawakilishi msimamo wa
Marekani’.
Ziara
ya Trump inajiri siku chache, baada ya taarifa kusema Trump alifichua taarifa
za siri kwa Warusi ambazo huenda zilitoka kwa mdokezi kutoka Israel.
Kisa
hicho kimeibua maswali kuhusu usiri na usalama wa habari za kijasusi
zinazokabidhiwa Marekani na Israel.
Operesheni
kubwa ya kiusalama inaendelea kabla ya ziara ya Trump, ambaye anatarajiwa
kukutana na Netanyahu mjini Jerusalem leo na kesho atakutana na kiongozi wa
Wapalestina, Mahmoud Abbas mjini Bethlehem.
Ajenda ya ziara ya Trump
Trump
pia atazuru Brussels, Vatican, naSicily. Ziara hiyo imegubikwa na mtafaruku wa
kisiasa nchini mwake, sana kutokana na hatua yake ya kumfuta kazi mkuu wa FBI
James Comey.
- Jumatatu -Jumanne, 22-23 Mei: Tel Aviv na Jerusalem, kabla ya kuzuru Ukingo wa Magharibi Jumanne
- Jumatano 24 Mei: Roma na Brussels. Bw Trump atakutana na Papa Francis, kisha viongozi wa Ubelgiji
- Alhamisi, 25 Mei: Mkutano wa Nato mjini Brussels
- Ijumaa, 26 Mei: Sicily, kwa mkutano wa G7
No comments