Header Ads

Trump akutana na Papa Francis



http://www.dw.com/image/38966106_303.jpg
VATICAN CITY, Vatican
RAIS wa Marekani, Donald Trump amekutana na Kiongozi wa Kiroho wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis. Viongozi hao mashuhuri ulimwenguni ambao mara nyingi hawakubaliani katika mambo kadhaa, wamekutana kwa mara ya kwanza mjini hapa.

Mkutano wao wa faragha uliodumu kwa dakika ambazo hazikutimia 30, ulimalizika kwa viongozi hao kupeana mikono mbele ya kamera za waandishi wa habari huku Rais Trump akimshukuru Papa Francis na kumwambia kuwa amefurahi na kwamba hiyo ilikuwa ni heshima kubwa aliyopewa kuweza kufika Vatican. 
Ziara ya Trump ilipangwa katika muda mchache, hali iliyosababisha kubadilika kwa mpangilio wa kazi wa Papa Francis ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 80.
Huu ni mkondo wa tatu katika safari ya kwanza ya nje ya Trump, ambapo alishazitembelea Saudi Arabia, Israel na Mamlaka ya Palestina. Trump na Papa Francis wana historia ambayo kwa kiasi kikubwa inatia hamu kutaka kuijua. 
Kwanza hawakubaliani na wamepingana hadharani katika masuala yanayohusu uhamiaji, uchu unaoletwa na ubepari, mabadiliko ya tabia nchi, adhabu ya kifo na biashara ya silaha.  Lakini wote wawili wanapinga juu ya kuhalalisha utoaji mimba.
Katika ziara hiyo, Trump aliandamana na mkewe Melania, binti yake Ivanka na mumewe Jared Kishner, msaidizi mkuu wa White House na mshauri wa masuala ya usalama.  Baada ya kumalizika mkutano shuguli ya kupeana zawadi ilifuata.
Papa Francis alifanya mazungumzo na wageni wake kwenye maktaba yake binafsi iliyopo katika ikulu ya Vatican, ambayo huwa haitumii mara nyingi. Rais Trump baada ya kukutana na Papa Francis alipanga kumpigia simu Rais wa Italia, Sergio Mattarella na Waziri Mkuu, Paolo Gentiloni.
Melania atazuru hospitali ya watoto na Ivanka Trump atafanya mazungumzo na wawakilishi wa jamii wa kidini wa St. Egidio, wanatarajiwa kujadili juu ya masuala yanayohusiana na uhamiaji na usafirishaji watu kinyume cha sheria.
Trump na timu yake walisafiri kuelekea Ubelgiji kwa ajili ya kukutana na maofisa wa Umoja wa Ulaya na wa Jumuiya ya kujihami ya NATO kabla ya kurejea Italia leo, ili kuhudhuria mkutano mkuu wa nchi za G7 utakaofanyika katika mji wa Sicily kuanzia Ijumaa na Jumamosi.

No comments

Powered by Blogger.