Nchi za Afrika zinazidi kustawi
RIPOTI iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika,
AfDB, kuhusu mustakabali wa ukuaji uchumi wa Afrika inaonesha kwamba Waafrika
wengi wanaona kuna ustawi katika hali za maisha yao.
Wakati idadi
kubwa ya wakaazi wa bara la Afrika karibu watu bilioni 1.2 wanaishi katika
umasikini, mataifa mengi kati ya 54 ya bara hilo yamepata mafanikio makubwa
katika nyanja za afya, elimu na hali ya maisha.
“Angalau
theluthi tatu ya nchi za Afrika zimepata mafanikio ya kati ya viwango vya juu
vya maendeleo ya binadamu,” imesema ripoti hiyo ya AfDB, ikimaanisha mkusanyiko
wa kipimo cha hali ya taifa.
Afrika
Kaskazini ina kiwango cha juu, ikikaribiana na viwango vya kimataifa, ambapo
Misri na Tunisia zinatajwa kuwa zina mfumo wa bima ya afya unaowafikia watu kwa
asilimia 75 kati ya 100.
Pia
kumeshuhudiwa mafanikio kadhaa katika mataifa mengine tangu kuanza kwa karne ya
21. Rwanda imetajwa kuwa nchi iliyopiga hatua zaidi katika mataifa yaliyo Kusini
mwa Jangwa la Sahara, ikifuatiwa na Ghana na Liberia, katika mapambano dhidi ya
umaskini tangu mwaka 2005.
Mojawapo ya
jitihada kubwa za Rwanda, ilikuwa ni mfumo wa huduma ya bima ya afya ya kijamii
ambapo hadi mwaka 2010, ilikuwa imewafikia watu tisa kati ya 10.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame
Matumizi katika elimu, suala ambalo linachukuliwa kuwa kigezo muhimu cha
maendeleo limefikia juu ya asilimia sita ya pato la taifa nchini Afrika Kusini,
Ghana, Msumbiji na Tunisia, lakini Nigeria, taifa lenye idadi kubwa zaidi ya
watu barani humo, inatumia chini ya asilimia moja ya pato lake la ndani katika
elimu.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, mataifa ya Umoja wa Ulaya
yanatumia wastani wa asilimia 4.9 ya pato la taifa katika elimu kwa mwaka 2013.
Afrika ya Kati, ambako viwango vya kuhitimu shule kwa wasichana ni vya
chini katika bara zima, pengo baina yao na wavulana linazidi kupungua. Idadi ya
wasichana waliomaliza sekondari kwa mwaka 2014 imefikia mara tatu zaidi tofauti
na muongo mmoja uliopita.
Usawa wa kijinsia umeongezeka katika mataifa kadhaa yakiwemo Botswana,
Namibia, Rwanda ambako wanawake wanafikia viwango sawa vya maendeleo ya
binadamu kama ilivyo kwa wanaume, imesema ripoti hiyo.
Mkuu wa Benki ya maendeleo ya Afrika Akinwumi Ayodeji Adesina
Licha ya hatua hizo, Waafrika milioni 544 wanaishi bado katika umaskini,
imesema ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha habari “Muonekano wa Kiuchumi wa
Afrika mwaka 2017,” ambapo bado changamoto nyingi zinasalia katika mapambano ya
vita dhidi ya umaskini.
Moja kati ya hizo ni ukosefu wa upatikanaji wa nishati ya kupikia, umeme
na usafi wa mazingira. Watu milioni 645 Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaishi
bila ya umeme.
Ripoti hiyo inasema kuwa mustakabali hauonekani kuwa mzuri kwa vijana
wadogo ambao wengi wao hawana ajira, kutokana na vijana hao kupatiwa elimu
isiyo na ujuzi sokoni.
Ripoti hiyo inatabiri kwamba yapo matumaini ya ukuaji wa uchumi kwa
asilimia 3.4 kwa mwaka huu, ikiwa ni ongezeko baada ya kukua kwa asilimia 2.2
mwaka jana.
Afrika Mashariki inasalia kuwa ukanda ulio na nguvu kiuchumi kwa bara
lote ikiongozwa na Ethiopia. Kwa ujumla Afrika iko nafasi ya pili katika ukuaji
duniani kote nyuma ya mataifa yanayoendelea ya Asia.
No comments