Header Ads

Marekani yawaonya washirika wa Korea Kaskazini



Nikki Harley
WASHINGTON DC, Marekani
BALOZI wa Marekani katika Umoja wa Mataifa (UN), Nikki Harley ameapa kuyataja mataifa yanaounga mkono Korea Kaskazini na mpango wake wa kinyuklia huku hali ya wasiwasi ikiendelea.

“Lazima uwe unaunga mkono Korea kaskazini ama unatuunga mkono, kwani kuendelea kuwaunga mkono wao (Korea Kaskazini) ni kukiuka vikwazo vya UN” alisema Harley.
Kauli hiyo ya Harley (pichani) inajiri kufuatia mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, uliofanyika jana kwa minajili ya kujadili ukiukwaji unaoendelea kufanywa na Korea Kaskazini.
Baraza hilo juzi Jumatatu kwa pamoja lilishutumu jaribio la kombora la masafa marefu lililotekelezwa na Korea Kaskazini na kuonya kuhusu vikwazo vipya.
Korea Kaskazini imesema kuwa kombora hilo lililofanyiwa majaribio, ni jipya na lina uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia. Lilisafiri urefu wa kilomita 700 na kwenda juu kilomita 2000 kabla ya kuanguka magharibi mwa bahari ya Japan. Hata hivyo Korea Kusini ilishindwa kubaini habari hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo jana, Harley aliyaonya mataifa yanayounga mkono Korea Kaskazini kuacha vitendo hivyo la sivyo yataona cha mtema kuni.
“Iwapo wewe ni taifa linalounga mkono Korea Kaskazini tutakutaja. Tutahakikisha kila mtu anajua wewe ni nani na tutakuwekea vikwazo hata wewe,” aliwaambia waandishi huku akiandamana na Balozi wa Japan na Korea Kusini katika umoja huo.
Harley alisema Marekani inaunga mkono mazungumzo na Korea Kaskazini, iwapo taifa hilo litasitisha majaribio ya makombora ya masafa marefu na yale ya kinyuklia.

No comments

Powered by Blogger.