Manula, Tshabalala, Niyonzima, Mexime watwaa tuzo za Ligi Kuu Tanzania

Mchezaji wa Simba SC, Mohammed Hussein
‘Tshabalala’ amefanikiwa kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara katika sherehe zilizofanyika usiku wa Jumatano ukumbi wa Mlimani
City, Dar es Salaam.
Tshabalala anayecheza upande wa beki wa kushoto, baada ya msimu mzuri akiiwezesha
Simba kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu nyuma ya mahasimu, Yanga
walioibuka mabingwa, amewabwaga Aishi Manula wa Azam, Simon Msuva wa Yanga, Shiza Kichuya wa Simba na Haruna
Niyonzima wa Yanga.
Lakini kiungo wa Rwanda, Niyonzima ‘akainua kwapa’
kwa kunyanyua tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni, akiwashinda beki Mzimbabwe wa
Simba, Method Mwanjali na beki Mrundi wa Mbao FC, Yusuph Ndikumana.
Manula naye akainua tuzo ya Kipa Bora akiwashinda
Owen Chaina wa Mbeya City na Juma Kaseja wa Kagera Sugar, wakati Msuva amebeba
tuzo ya Mfungaji Bora kwa pamoja na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting baada ya
wote kufungana kwa mabao 14 kila mmoja.
Mecky Mexime amewashinda makocha wa kigeni, Mcameroon wa Simba, Joseph Omog na Ettiene Ndayiragije wa Mbao FC. Mshambuliaji chipukizi wa Kagera Sugar, Mbaraka Yussuf Abeid ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu akiwaangusha Shaaban Iddi wa Azam FC na Mohammed Issa ‘Banka’ wa Mtibwa Sugar.
Shaaban Iddi naye akawaangusha mchezaji mwenzake wa Azam, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ na Mosses Kitambi wa Simba katika tuzo ya Mchezaji Bora wa U-20, inayojulikana kama tuzo ya Ismail Khalfan wakati Shiza Kichuya akashinda tuzo ya Bao Bora la Msimu alilofunga kwenye mechi dhidi ya Yanga katika ushindi wa 2-1 akiyazidi mabao ya Peter Mwalyanzi wa African Lyon na Zahoro Pazi wa Mbeya.
Refa Bora ni Elly Sasii wa Dar es Salaam
aliyewashinda Shomari Lawi wa Kigoma na Hance Mabena wa Tanga, wakati Tuzo
ya Heshima imekwenda kwa gwiji Kitwana Manara aliyeanza kucheza kama kipa na
baadaye mshambuliaji kwa mafanikio makubwa timu ya taifa na klabu ya Yanga na
Mwadui FC imeshinda tuzo ya timu yenye Nidhamu.
No comments