Daraja la Magara kuanza kujengwa Julai mwaka huu
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), mkoa wa Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa, akifafanua jambo kwa Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, wakati
alipokuwa akikagua mahali ambapo litajengwa Daraja la Magara lenye urefu wa meta
84, wilayani Babati, mkoani Manyara, jana.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Christopher
Saul (katikati), kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), mkoa wa Manyara
wakati alipokuwa akikagua mahali ambapo litajengwa Daraja la Magara lenye urefu
wa meta 84, Wilayani Babati, mkoani humo, jana.
Mwonekano wa sehemu ambapo Daraja la
Magara lenye urefu wa meta 84 katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani-Mbulu yenye
urefu wa kilomte 21 litakapojengwa. Mkataba wa ujenzi wake unatarajiwa
kusainiwa mwezi Juni mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha
Mayoka kuhusu mkakati wa Serikali katika ujenzi wa Daraja la Magara wilayani
Babati, mkoani Manyara, jana.
Serikali imesema ipo katika hatua za
mwisho za kumpata mkandarasi atakayejenga Daraja la Magara lenye urefu wa meta
84 katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani-Mbulu yenye urefu wa kilometa 21
lililopo mkoani Manyara ambapo mkataba huo unatarajiwa kusainiwa Juni mwaka
huu.
Akizungumza hayo jana kwa wananchi wa
Kijiji cha Mayoka, wilaya ya Babati, mkoani humo, Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, aliwataka wananchi hao kutoa
ushirikiano kwa mkandarasi atakayepatikana ili kurahisisha mradi huo kukamilika
kwa wakati.
“Serikali inaendelea kukamilisha taratibu
zake ili kumpata mkandarasi, sasa ombi langu kwenu ni kuhakikisha kuwa mnatoa
ushirikiano kwa mkandarasi huyo pindi atakapofika eneo la kazi,” alisema Ngonyani.
Alibainisha kuwa Serikali imekuwa
ikitenga fedha mwaka hadi mwaka, ili kuweza kukamilisha mradi huo ambapo kwa
mwaka wa fedha 2017/18 zaidi ya Sh. bilioni 1 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa
kilometa 1.2 za barabara sehemu ya mlima Magara ambayo itajengwa kwa kiwango
cha zege.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara
nchini (TANROADS), mkoa wa Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa alimhakikishia
Naibu Waziri huyo kumsimamia mkandarasi atakayepatikana katika ujenzi wa daraja
hilo ili kuondoa kero na adha wanayopata wakazi wa Babati na maeneo jirani.
Aliongeza kuwa ujenzi wa daraja la
Magara, pia utahusisha ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2
kwa kiwango cha lami na kilometa 2 kwa kiwango cha Changarawe.
Daraja la Magara ni moja ya daraja
litakaloleta chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Arusha, Mbulu na Babati, kwani
ujenzi wake utarahisisha huduma za usafirishaji na kukuza utalii kwa nchi
kupitia Hifadhi ya Mbuga ya Manyara.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments