Header Ads

Zuma: Wanaoandamana kunipinga ni wabaguzi wa rangi



Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma
PRETORIA, Afrika Kusini
RAIS Jacob Zuma (pichani) amewataja watu wanaofanya maandamano dhidi yake kuwa wabaguzi wa rangi, huku akiongeza kuwa walibeba mabango yaliyoonesha kuwadharau watu weusi.

Maelfu ya waandamanaji walifanya maandamano baada ya Zuma kumfuta kazi Waziri wa Fedha, Pravin Gordhan. Maandamano hayo yalipangwa na vyama kadhaa vya upinzani na makundi ya wanaharakati.
“Maandamno yaliyofanyika wiki iliopita, yalibainisha kwamba ubaguzi wa rangi upo na unaendelea nchini,” alisema.
Wakati huohuo, wafuasi wa Zuma walivuruga hafla ya makumbusho ya aliyekuwa mwanaharakati wa kupambana na ubaguzi wa rangi, Ahmed Kathrada.
Watu hao walianza kuleta uzushi wakati Gordhan alipokuwa anatoa hotuba yake ambayo ilikuwa inakashifu ufisadi katika chama cha ANC, akisema kuwa huenda chama hicho hakitashinda uchaguzi wa 2019.
Umati ulianza kuimba nyimbo za kumsifu Zuma ambaye amekumbwa na kashfa baada ya nyingine. Hafla hiyo ya Kathrada ilikuwa ikiendelea KwaZulu-Natal, ambapo umati huo ulimsifu Zuma kwa kumpiga kalamu Gordhan.
Akijaribu kuipaza sauti yake juu ya kelele wa umati, Gordan alisema; “ikiwa tutaendelea kuzozana tutapoteza imani ya watu wa Afrika Kusini kwetu. Tunataka kubaki serikalini ili tuibadilishe Afrika Kusini.”
Waandamanaji wanaopinga uongozi wa rais Zuma 
Waandamanaji wakiwa na mabango ya kumpinga Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.
Wiki ijayo, Zuma anatarajiwa kupambana na kura ya kutokuwa na imani dhidi yake ambayo inasimamiwa na upinzani. Anadaiwa kuwa kiongozi fisadi ambaye anataka kuwajaza rafiki zake kwenye wizara ya fedha.
Rafiki zake Zuma wanakanusha madai hayo kwa kusema kwamba Zuma ana nia tu ya kuendeleza mabadiliko makubwa ya kiuchumi yatakayonufaisha nchi.
Mahakama ilitoa amri mwaka jana ikisema kuwa Zuma alivunja kiapo chake cha kazi kwa kukosa kulipa serikalini, fedha zilizotumiwa kuboresha makazi yake ya binafsi na kutaka ashtakiwe kwa kosa la ufisadi. Zuma anasema yeye hana makosa yoyote.
BBC

No comments

Powered by Blogger.