Watano wafariki shambulio la kigaidi Westminister
Polisi wakiwapatia huduma za kwanza majeruhi wa tukio la kigaidi
lililotokea jana katika eneo la Bunge la Westminister.
LONDON, Uingereza
WATU watano wamethibitishwa kufariki dunia na
wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa, baada ya mshambuliaji kuvurumisha gari na
kuwagonga watu katika daraja la Westminister jijini hapa.
Mara baada ya kugonga kwa gari, shambuliaji huyo
kisha alimdunga kisu ofisa wa polisi lakini akauawa kwa kupigwa risasi na
polisi katika maeneo ya Bunge. Ofisa wa polisi aliyeuawa ametambuliwa kwa
majina ya Keith Palmer, 48.
Waziri Mkuu, Theresa May amesema shambulio hilo
lilikuwa ‘la ukosefu wa maadili’ na lilishambulia maadili makuu ya uhuru wa
kufanya maamuzi, demokrasia na uhuru wa kujieleza. Polisi hawajafichua jina
wala maelezo zaidi kumhusu mshambuliaji.
May alishutumu shambulio hilo na kusema juhudi kama
hizo za kuvuruga maadili ya Uingereza hazitafanikiwa.
Aliwashukuru maafisa wa polisi waliofika eneo hilo
baada ya tukio na kusema: "Sote tutasonga mbele pamoja, hatutayumbishwa na
ugaidi na hatutakubali chuki na uovu kututenganishwa. Haikuwa ajali kwamba
shambulio hili lilitekelezwa eneo hili.
"Gaidi huyu aliamua kushambulia katikati mwa
jiji kuu ambapo watu wa mataifa yote, dini zote na tamaduni zote hukusanyika
kusherehekea maadili ya uhuru wa maamuzi, demokrasia na uhuru wa
kujieleza."
May anatarajiwa kutoa hotuba baadaye leo katika
Bunge la Commons.
Kaimu Naibu Kamishna wa Polisi ambaye anasimamia
kitengo cha kukabiliana na ugaidi katika Polisi wa Jiji Kuu, Mark Rowley
amesema anafikiria wanamfahamu mshambuliaji na kwamba huenda alihamasishwa na
makundi ya kigaidi ya kimataifa yenye uhusiano na itikadi kali za Kiislamu.
Hata
hivyo, hakutoa maelezo zaidi. Shambulio hilo lilitokea majira ya saa 14.40
(nane na dakika arobaini mchana kwa Uingereza) GMT jana, baada ya mshambuliaji
mmoja aliyekuwa na gari la rangi ya kijivu aina ya Hyundai i40 alipolivurumisha
gari hadi eneo la kutumiwa na wanaotembea kwa miguu kwenye Daraja la West
Minister, karibu na Majengo ya Bunge.
Aliwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine wengi. Baadaye
aligongesha gari lake kwenye uzio nje ya Majengo ya Bunge. Baada ya matukio
hayo, mshambuliaji huyo alikimbia, akiwa na kisu, hadi kwenye jengo la Bunge
ambapo alikabiliwa na polisi.
Palmer ambaye hakuwa na silaha, alidungwa kisu na
mshambuliaji huyo alifariki baadaye. Mshambuliaji huyo alipigwa risasi na
kuuawa na polisi waliokuwa na silaha hapo karibu.
Rowley alitoa heshima zake kwa Palmer, na kusema: “Ni
mtu aliyetoka kwake nyumbani leo kwenda kazini akitarajia kurejea nyumbani
baada ya kumaliza zamu yake, na alikuwa na kila haki kutarajia kwamba hilo
lingefanyika.”
Waziri wa Mambo ya Nje, Tobias Ellwood, mwanajeshi
wa zamani ambaye kaka yake aliuawa katika shambulio la kigaidi la Bali mwaka
2002, alijaribu kumpa Palmer huduma ya kwanza.
Mwanamke mmoja alifariki baada ya kugongwa na gari
la mshambuliaji huyo kabla ya gari hilo kufika eneo la majengo ya Bunge. Alithibitishwa
kufariki na daktari katika hospitali ya St Thomas'.
BBC
No comments