MAFUNZO JUU YA MWONGOZO WA USIMAMIZI WA UWEKEZAJI WA UMMA YAFUNGULIWA CHUO CHA MIPANGO DODOMA
Na Thomas Nyindo.
Maofisa wa Idara za Sera na Mipango kutoka Wizara, Idara na Wakala za
Serikali wametakiwa kuongeza ufanisi na ubunifu katika kuandaa na kusimamia
miradi ya maendeleo ili kuharakisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya
Mipango, Bw. Maduka Kessy wakati akifungua mafunzo ya Mwongozo wa Usimamizi wa
Uwekezaji wa Umma yanayoendelea katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.
Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo maofisa
wanaosimamia masuala ya Sera na Mipango katika kuibua na kutekeleza miradi ya
maendeleo, hususan, ile inayogharamiwa kwa fedha za Serikali ili kufanya
Tanzania kuingia kwenye nchi za kipato cha kati kama ilivyoaninishwa kwenye
Dira ya Taifa ya Maendeleo.
“Mipango ya maendeleo tunayojiwekea, kama taifa, inapaswa kutafsiriwa
katika miradi na programu za utekelezaji, hivyo mafunzo haya yatatusaidia
kuongeza ufanisi, ubunifu na uwajibikaji katika kuandaa miradi na kusimamia
miradi yenye tija kwa wananchi,” alisema Kessy.
Aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuwa wao ni miongoni mwa wadau
muhimu katika kuifanya Tanzania ipige hatua za maendeleo kwa kuwa ndio
wanaohusika katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, Kessy alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kuongeza
ufanisi na ubunifu katika kuchagua miradi, kutafuta fedha za ugharamiaji na
kuboresha uratibu wa kufungamanisha uwekezaji wa umma kwa kubainisha
hatua za kufuata katika kujumuisha miradi ya maendeleo katika bajeti za
maendeleo.
“Mwongozo huu utawasaidia kufanya maamuzi katika kuchagua miradi sahihi
ya uwekezaji katika sekta ya umma na kuhakikisha ufanisi katika utekelezaji
wake. Sote tunafahamu kuwa azma yetu ya maendeleo kitaifa ni kufikia uchumi wa
kipato cha kati ifikapo 2025,” alisema.
Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza kuwa zipo changamoto zinazokabili
usimamizi wa miradi ya maendeleo, kuanzia hatua ya kubuni, kutekeleza hadi
kukamilisha miradi hiyo. Kwa hiyo Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji waRasilimali
za Umma ni mojawapo ya maandiko muhimu ambayo yamebuniwa kukabiliana na
changamoto hizo.
Mgeni
Rasmi Bw. Maduka Paul Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango
(aliyesimama) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi
wa Uwekezaji wa Umma kwa washiriki kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea
na Wakala za Serikali. Wengine ni Bi. Lorah Madete, Kaimu Naibu
Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla, Tume ya Mipango (kulia) na Bw. John
Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kushoto).
Washiriki
wa Mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mgeni Rasmi (hayupo pichani) wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo.
Dkt.
John Mduma, Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (aliyesimama),
akitoa neno kwa washiriki wa mafunzo mara baada ya mafunzo hayo kufunguliwa
rasmi.
Washiriki
wa mafunzo kuhusu Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma kutoka Idara za Sera na Mipango za Wizara, Idara zinazojitegemea
na Wakala za Serikali pamoja na
wawezeshaji wa mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni
Rasmi mara baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
No comments