‘Korea Kaskazini ina mpango wa kushambulia kisiwa cha Marekani’

SEOUL- KOREA Kaskazini imedokeza kwamba, inatafakari
uwezekano wa kurusha makombora karibu na jimbo la Marekani la Guam katika
bahari ya Pasifiki, saa chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kulitishia
taifa hilo kuwa litakabiliwa kwa ‘moto na ghadhabu’.
Shirika la
habari la Serikali ya Korea Kaskazini (KCNA), limesema taifa hilo linatafakari
mpango wa kurusha makombora ya masafa ya kati na marefu karibu na Guam, eneo
ambalo Marekani huwa na ndege zake za kuangusha mabomu.
Taarifa hiyo,
inaashiria kuongezeka kwa uhasama kati ya nchi hizo mbili kutokana na
kuidhinishwa kwa vikwazo vipya. Hivi karibuni, Umoja wa Mataifa (UN) iliidhinisha
vikwazo zaidi vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo.
Rais Trump
ametoa tamko lake baada ya ripoti kwenye vyombo vya habari kusema kwamba, Korea
Kaskazini imeweza kuunda kichwa cha silaha za nyuklia chenye uwezo wa kutosha
kwenye makombora yake.
Ufanisi huo,
ingawa haujathibitishwa rasmi, ulitazamwa na wengi kama kiunzi cha mwisho
kilichoizuia Korea Kaskazini kuwa taifa kamili lenye nguvu za silaha za
nyuklia.
Taarifa ya
gazeti la Washington Post, ikunukuu maofisa wa ujasusi wa Marekani, imedokeza
kwamba Korea Kaskazini inaunda silaha za nyuklia zenye uwezo wa kuishambulia
Marekani kwa kasi zaidi ya ilivyotarajiwa.
(KCNA
limesema jeshi la nchi hiyo linachunguza kwa makini mpango wa kuanzisha moto wa
kuzingira Guam kwa kutumia makombora ya roketi ya masafa ya wastani na ya
masafa marefu ya Hwasong-12.
Shirika hilo
limesema mpango huo utawasilishwa kwa Viongozi Wakuu, baada ya ‘kutathminiwa
kwa kina na kukamilishwa’ na utatekelezwa kiongozi wake Kim Jong-un akiamrisha.
Kisiwa cha
Guam kina ukubwa wa kilomita mraba 541 (maili mraba 209) na kinapatikana bahari
ya Pasifiki kati ya Ufilipino na Hawaii.
Ni jimbo ‘lisilo
na mpangilio wowote, na lisilojumuishwa kikamilifu’ la Marekani, lenye wakazi
karibu 163,000.
Kambi za
jeshi la Marekani hutumia karibu robo ya ardhi ya kisiwa hicho. Marekani ina
wanajeshi 6,000 kisiwa hicho na kuna mipango ya kuwasafirisha maelfu wengine
huko.
Ni kituo
muhimu katika shughuli za kijeshi za Marekani, ambapo huwezesha wanajeshi wa
nchi hiyo kufika maeneo mengi muhimu Pasifiki, mfano eneo la bahari
linalozozaniwa la South China Sea, rasi ya Korea na mlango wa bahari wa Taiwan.
Majibizano
kati ya Marekani na Korea Kaskazini yamezidi, baada ya Pyongyang kufanyia
majaribio makombora mawili yenye uwezo wa kusafiri kutoka bara moja hadi jingine,
na kudai sasa ina makombora yanayoweza kufika Marekani.
Trump aliwaambia
wanahabari Jumanne kwamba; “Korea Kaskazini wasidhubutu kutoa vitisho zaidi kwa
Marekani. Watajibiwa kwa moto na ghadhabu ambayo ulimwengu haujawahi
kushuhudia.”
Seneta
mkongwe wa Marekani, John McCain hata hivyo alikuwa na shaka kuhusu tamko la
Trump.
“Viongozi
wengi wakuu ambao nimewahi kuwaona, huwa hawatoi vitisho ikiwa hawako tayari
kuvitekeleza na sina uhakika kwamba Rais Trump yuko tayari kuchukua hatua,”
alisema McCain.
Korea
Kaskazini ilighadhabishwa na vikwazo vipya ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa
siku ya Jumamosi. Vikwazo hivyo vina lengo la kupunguza mapato kutoka kwa mauzo
ya bidhaa nje ya Korea Kaskazini kwa theluthi moja.
KCNA imesema
Korea Kaskazini, ambayo imefanyia majaribio silaha za nyuklia mara tano,
itajibu vikali na kwamba ‘Marekani italipia’ kwa kuchangia kutunga vikwazo
hivyo.
BBC
No comments