Ndumbaro huru kifungo cha TFF
SHIRIKISHO
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kumfutia kifungo cha miaka saba
cha kutojihusisha na masuala ya soka, Wakili Damas Ndumaro aliyefungiwa zaidi
ya miaka miwili iliyopita.
Uamuzi huo
wa Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF ulitangazwa na mwenyekiti wake, Rahim
Shaban Zuberi kwenye ofisi za TFF zilizopo Karume jijini Dar es Salaam, jana.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Zuberi alisema kamati yao imefikia uamuzi huo kutokana na
Ndumbaro kuomba kufanyiwa marejeo kwa hukumu yake, na wao walibaini hakupata
nafasi ya kujitetea huku pia baadhi ya mambo hayakuzingatia usawa wakati
akifungiwa.
Awali
Ndumbaro alihukumiwa mwaka mmoja kwa kosa la kwanza kutoa taarifa zisizo sahihi
kiasi cha kupotosha uamuzi wa TFF kinyume cha kanuni nambari 41 kifungu kidogo
cha sita cha kanuni za Ligi toleo la mwaka 2014.
Pia,
alifungiwa miaka saba kwa kosa la pili, ambalo ni kushawishi au kupotosha na
kuzuia uamuzi wa TFF kupitia bodi ya Ligi kinyume cha kanuni ya nne kifungu kidogo
cha 16 toleo la mwaka 2014.
Ndumbaro
alisema klabu 12 za Ligi Kuu zilimwomba kuwawakilisha kupinga makato ya
asilimia tano za fedha za udhamini wa Ligi Kuu, wakati klabu nyingine zilikana
kuhusika na mpango huo, Coastal Union na Stand United.
Ndumbaro
alikuwa ametumikia adhabu yake kwa muda wa miaka miwili na miezi tisa.
Kamati hiyo
pia imemwachi huru aliyekuwa kocha wa timu ya Geita Gold Mine, Choke Abeid kuendelea na shughuli za soka, ambaye awali
alifungiwa maisha kutokana na tuhuma za kupanga matokeo katika mchezo dhidi ya
JKT Kanembwa msimu wa 2015-16.
“Lakini
kamati pia ilipitia rufaa za watu wengine waliohukumiwa kutojihusisha na soka
wakiwemo Yusuph Kitumbo, Fatch Rhemtullah na Thomas Mwita, hawa adhabu yao
itaendelea kama ilivyo mwanzo,” alisema Zubery
Hukumu hiyo
imetoka siku mbili baada ya kamati hiyo , chini ya mwenyekiti wake, Tarimba
Abass kumfutia adhabu Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji
Manara adhabu ya kufungiwa kutojihusisha na soka kwa kipindi cha miezi 12 na
kulipa faini ya sh milioni 9.
Mbali na
Manara, kamati hiyo pia iliwafutia adhabu Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira
wa Miguu Rukwa, Blassy Kiondo na mwenyekiti wake Ayubu Nyaulingo na Mwenyekiti
wa Kamati ya Uchaguzi Rukwa ambao walikuwa wamefungiwa kutokana na kufanya
uchaguzi wakati TFF iliwazuia.
No comments