Tunasubiri maajabu ya Benki ya Kilimo
Julian Msacky
SERIKALI ya Awamu ya Tano imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
viwanda ili kufikia uchumi wa kati.
Ndiyo maana viongozi wa serikali na sekta binafsi wanahimiza watu wajikite
katika sekta hiyo ili kuikwamua nchi kiuchumi.
Tunavyofahamu ni kwamba ili kufikia huko lazima sekta ya kilimo
iwezeshwe kwa kila mbinu ili iweze kufanya kazi kwa tija.
Kusema kweli bila kuwekeza katika sekta ya kilimo chini ya kaulimbiu ya
Hapa Kazi Tu ni vigumu kuwa nchi ya kiviwanda.
Hii ni kwa sababu kuna uhusiano wa karibu kati ya viwanda na kilimo ili
Taifa liweze kuwa na uchumi imara kwa nchi na watu wake.
Ni katika kuwekeza maeneo hayo tutaweza kupunguza umaskini nchini na
kupanua wigo wa ajira kwa Watanzania wengi.
Kwa hiyo viongozi wetu wanapohubiri suala la viwanda ni lazima
wahakikishe pia kwamba sekta ya kilimo imewezeshwa vilivyo.
Ili wakulima walime kwa tija wanahitaji kuwezeshwa na kupatiwa nyenzo
zinazotakiwa ili kutuondoa hapa tulipokwama.
Ni lazima tukiri pia kwamba enzi za uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere
kilimo kilithaminika mno kwa sababu uongozi ulikithamini.
Watu wengi walibaki vijijini wakifanya shughuli za kilimo na hakika
wimbi la vijana kukimbilia mijini lilikuwa dogo mno.
Lakini siku hizi vijana wamefurika mijini kwa sababu vijiji si sehemu
rafiki kwao. Wanaona usalama wa maisha
yao upo mijini.
Swali ni je, serikali imejipanga inavyotakiwa kuhakikisha kilimo chetu kinaboreshwa
kama enzi za Mwalimu Nyerere?
Je, wataalamu wa kilimo wapo vijijini wakielekeza wakulima nini walime
na katika ardhi gani ili tuzalishe kwa ufanisi?
Tumejipangaje kuwapatia wakulima mikopo rahisi na ruzuku ili wafufue
mazao waliotelekeza kwa vile hakiwalipi?
Hebu tuone. HIVI karibuni Wizara ya Fedha na Mipango iliipatia Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) sh. bilioni 209.5.
Tumeambiwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiongezea mtaji ili kukidhi
malengo ya kutoa mikopo kwa wakulima wa kati na wadogo.
Ndivyo alivyotuambia Naibu Katibu Mkuu wa Waziri hiyo, Dk Khatibu
Kazungu akisema wameongeza mtaji TADB ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango
wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/2021 ili kuboresha sekta ya kilimo.
Kaimu Mkurugenzi wa benki hiyo, Francis Assenga anasema fedha hizo
zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na hadi sasa wamefikia wakulima 3700
tangu ilipoanzishwa.
Nikiri tu hapa kuwa kuanzishwa kwa benki hii ni jambo jema. Ni hatua
muhimu ya kuhakikisha tunawezesha wakulima kimtaji.
Katika hili niseme mambo kadhaa ambayo pengine yakizingatiwa itasaidia
nchi kufanya vitu vya kwa mpangilio na tija zaidi.
Mosi, benki ikitumiwa vizuri na kutoa elimu kwa walengwa tutaona
mabadiliko ya haraka katika sekta yetu ya kilimo.
Hii ikiwa na maana kuwa wakulima waoneshwe fursa hiyo hasa vijijini.
Benki hii isitumie muda wake mwingi maeneo ya mijini.
Maofisa wake waendee vijijini, waelimishe wakulima taratibu za kukopo
na waelimishwe aina ya mazao yenye tija kwao.
Benki hii inatakiwa iwe mwarobaini wa kuinua kilimo nchini hasa mazao
ya biashara kwani kwa sehemu kubwa ni kama vile yamekufa.
Ni wapi leo hii utaona wakulima wakichangamkia kilimo cha kahawa,
pamba, chai, katani au korosho kama ilivyo zamani?
Ingefurahisha kama benki hiyo ingetumika zaidi kuwekeza kwenya mazao
hayo na kuhakikisha tunazalisha kwa ufanisi.
Kilichoua mazao hayo ni gharama kubwa za uendeshaji na wakulima
kunyonywa bei wakati wanapouza na kuona haina maana tena kulima.
Sasa benki hiyo iamshe upya ari ya wakulima kulima mazao hayo.
Tukifanya hivyo kwa hakika Watanzania wengi watakimbilia huko.
Wataacha tabia ya kuzunguka mjini na viatu viwili wakitafuta wateja kwa
sababu wimbi la wamachinga “tumelitaka sisi wenyewe”.
Kwa maana hiyo wa kuliondoa ni sisi wenyewe. Njia nzuri ni mosi,
kuwekeza vizuri kwenye sekta ya kilimo ili kithaminiwe.
Hivyo Benki ya Kilimo ina nafasi kubwa kututoa hapa tulipokwama kwa
miongo kadhaa sasa hususan kwenye sekta ya kilimo.
Tunaamini maofisa wa benki hiyo watajipanga vizuri na kuhakikisha
inaleta mabadiliko chanya kwa wakulima wetu.
Sekta hiyo imezirai kwa muda mrefu na wakulima wamekata tamaa kwa muda
mrefu, hivyo benki hiyo iwaondoe Watanzania hapo.
Kama kweli tunaamini kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu tuoneshe
hivyo kwa vitendo maana ardhi ipo pamoja na rasilimali watu.
Tunasubiri kuona maajabu ya benki ya kilimo kwa wakulima wetu, lakini
nisisitize kuwa tukishindwa tena wakati huu hatutaweza tena.
Hii ni kwa sababu wakulima wetu wameteseka kwa muda mrefu hivyo
wanahitaji faraja na faraja yenyewe ni kuwezeshwa.
Waendeshe kilimo cha kisasa, kilimo cha umwagiliaji kama wanavyofanya
wenzetu wa Misri badala ya kutegemea mvua tangu Uhuru.
Wiki ijayo tutaangalia namna ya kutumia
rasilimali zetu kutokana na mahitaji ya nchi.
msackyj@yahoo.co.uk,
0718981221
No comments