Zuma adaiwa kuwa na mpango wa kuhamia Dubai

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
HALI imezidi kuwa tete kwa Rais Jacob Zuma, baada ya kuibuka kwa kashfa
mpya ambapo wakosoaji wake wameeleza kwamba ana mpango wa kuhamia Dubai kwa
ajili ya kuishi huko hivi karibuni.
Hayo yanajiri, baada ya kubainika kwa mawasiliano kupitia barua pepe ambazo
zimechapishwa na gazeti moja nchini, zinazoonesha uhusiano mkubwa kati ya Rais Zuma
na familia yenye utata ya Gupta, kuhusu madai hayo ya kuhamia Dubai.
Wakati chama tawala nchini cha ANC kikikumbwa na vita vya ndani kwa
ndani, barua pepe hizo zinatarajiwa kuibua mjadala mkali kwani zinafichua
mipango ya Rais Zuma wa kuhamia Dubai.
Barua pepe hizo baina ya mwanawe wa kiume, Duduzane, na vigogo wa kampuni
inayomilikiwa na familia ya Gupta, zinashirikisha barua moja iliyotumwa kwa
familia ya kifalme mjini Dubai, ambapo Zuma anasema angetaka kuwa na makao ya
pili huko Dubai.
Madai hayo yanaibua mjadala
wa iwapo Rais Zuma anajiandaa kubwaga manyanga, kwani chama chake nacho kinaonekana
kumgeuka.
Hata hivyo, madai hayo
yamekanushwa vikali na Msemaji wa Rais Zuma, ambaye amepuuza barua pepe hizo na
kudai kuwa ni uvumi na uchokozi kwa kiongozi huyo.
Hayo yakiarifiwa, ombi la
kutokuwa na imani na Rais Zuma limewasilishwa kwa Kamati Kuu ya chama cha ANC
inayokutana mjini Pretoria ikiwa ni mara ya pili kwa ombi hilo kuwasilishwa.
Wanachama wa ANC ambao wanampinga Rais Zuma, kwa mara nyingine tena
wanajaribu turufu yao, lakini huenda wanchama wa kamati hiyo watiifu kwa Zuma
wakaangusha muswada huo.
Mbali na kuwasilishwa kwa maombi hayo kwa kamati kuu, bado kuna kesi
inayoendelea katika Mahakama ya Katiba iwapo wabunge wataruhusiwa kura ya siri ya kwa muswada wa kutokuwa na
imani na Zuma. Kamati hiyo inatarajiwa kuamua atakayemridhi Zuma ifikapo Desemba
mwaka huu.
No comments