Jukwaa la Haki na Usalama kugawa vitabu 7,000
Ofisa Elimu Maalum wilaya Ilala, Salehe Msechu wa
pili kutoka kulia akionesha kitabu cha nukta nundu, ambaye alikuwa mgeni rasmi
katika hafla ya kukabidhi vitabu 20 vya nukta nundu ambao ni kwa aajili ya
wanafunzi wasiona katika Shule ya Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam, wa
kwanza kushoto ni Mjumbe wa Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Madeline Kimei, akifuatiwa na Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wasiona
Tanzania Jonas Lubago na wa mwisho ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Anna
Mshana
Suleiman Msuya
JUKWAA la Haki na Usalama linatarajia
kugawa vitabu 7,000 ambavyo vimebeba ujumbe kuhusu mambo 101 mwananchi anapaswa
kuyajua kuhusu polisi huku vitabu 300 vikilenga watu wenye mahitaji maalum.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Baraza la
Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Madeline Kimei wakati akizindua
na kukabidhi vitabu 20 vya nukta nundu kwa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko
iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam jana.
Alisema TLS imejipanga kugawa vitabu
hivyo ambayo vitasaidia jamii ambayo imekuwa ikikutana na changamoto mbalimbali
wakati ikikutana na polisi.
Kimei alisema TLS kwa kushirikiana na
Jukwaa la Haki na Usalama imeweza kuandaa machapisho manne yanayohusu polisi
ambapo mawili ni nyaraka za majadiliano ambayo inahusu uhuru wa kioperesheni na
uwajibikaji wa jeshi hilo.
Alisema mengine mawili ni vitabu vya
kutoa uelewa kwa wananchi juu ya polisi na mbaraza ya usalama ya wilaya ambapo
mwitikio umekuwa mkubwa.
“Siku ya leo tuko hapa kwa ajili ya
kuzindua toleo la nukta nundu la moja wapo ya vitabu vilivyochapishwa chini ya
mradi huu ambapo kitabu hiki kinaitwa “mambo 101 unayoyahitaji kuyafahamu juu
ya polisi lakini unaogopa kuyauliza,” alisema.
Mjumbe huyo alisema uandaaji wa vitabu
vya nukta nundu unagharama kubwa lakini kutokana na wao kutambua umuhimu wa
kundi hilo wamelazimika kuchapisha vitabu 300 kwa kuanzia katika kundi hilo.
Alisema lengo kuu ni kuhakikisha kuwa
wananchi wote wantambua kazi za polisi jinsi zinavyofanywa na changamoto ambazo
wanakutana nazo.
Kimei alisema kitabu hicho kitaelimisha
jamii jinsi jeshi hilo linavyofanya kazi na ukomo wake wa madaraka hivyo kila
pande kutekeleza majukumu yake kwa haki.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo Ofisa
Elimu Maalum Wilaya ya Ilala, Salehe Msechu alisema uamuzi wa Jukwaa la Haki na
Usalama ni wa kuungwa mkono na jamii huku akisisitiza wadau wengine kujitokeza
kusaidia.
Msechu alisema Serikali imejipanga
kusaidia kundi la watu maalum hivyo itajitahidi kutoa vifaa mbalimbali ambavyo
vitatumika kwa wanafunzi katika wilaya hiyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Mchanganyiko, Anna Msechu alisema shule hiyo ina wanafunzi 69 wasiona hivyo
vitabu hivyo vya nukta nundu vitasaidia kuatua tatizo.
“Hapa nina wanafunzi 69 ambao
watafaidika na vitabu hivi havikidhi hitaji lakini vitasaidia kwa kiasia fulani
tunaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wasiona
Tanzania, Jonas Lubago alisema vitabu vya watu wa elimu maalum hasa wasiona kwa
Tanzania vinapatikana kwa chini ya asilimia mojo hivyo jitihada zinahitaji ili
kukidhi hitaji.
Mwisho
No comments