Header Ads

Aliyekuwa rais Korea Kusini Park Geun-hye 'kukamatwa'



Park Geun-hye
SEOUL, Korea Kusini
WAENDESHA Mashtaka nchini, wamesema wataomba idhini ya kumkamata aliyekuwa rais ambaye aliondolewa madarakani, Park Geun-hye, kwa mchango wake katika kashfa ya ulaji rushwa.

Park (pichani) alipoteza kinga ya rais dhidi ya kufunguliwa mashtaka mapema mwezi huu na akaondolewa rasmi madarakani baada ya Mahakama ya Katiba kudumisha uamuzi wa bunge wa kumng'oa madarakani.
Park anatuhumiwa kumruhusu rafiki yake wa karibu Choi Soon-sil kudai fedha kwa lazima kutoka kwa kampuni kubwakubwa. Hata hivyo, Park alikanusha madai hayo na kisha kuomba radhi kwa umma wiki iliyopita, kabla ya kuhojiwa na maofisa wa mashtaka kwa saa 14.
Waendeshaji mashtaka leo walisema kwamba ‘wameamua kwamba ni vema, kwa kufuata sheria na maadili nchini, kuomba kibali cha kumkamata’.
Wanasema ushahidi, ambao unapatikana katika diski za kompyuta huenda ukaharibiwa iwapo Park hatakamatwa. Choi amefunguliwa mashtaka ya ulaji rushwa na tayari kesi dhidi yake imeanza.
Park aling'olewa vipi madarakani?
Park aliondolewa madarakani kutokana na uhusiano wake wa karibu na Choi. Choi anatuhumiwa kutumia uhusiano wake na rais huyo kushinikiza kampuni kutoa mamilioni ya dola kama mchango kwa wakfu za kusaidia jamii ambazo alikuwa anazisimamia.
Kaimu mkuu wa kampuni kubwa ya vifaa vya kielektroniki ya Samsung, Lee Jae-yong, alikamatwa kuhusiana na kashfa hiyo. Park, 65, anadaiwa kuhusika moja kwa moja katika hili, na kwamba alimruhusu Choi uhuru wa kiwango kisichokubalika wa kufikia nyaraka rasmi za serikali.


No comments

Powered by Blogger.